Mwanamfalme ahusishwa kutoweka mwandishi

Mwanamfalme Mohammed bin Salman

Muktasari:

  • Picha zimekuwa zikimwonyesha mtuhumiwa huyo akionekana akishuka kwenye ndege katika ziara za Mwanamfalme jijini Paris, Ufaransa na Madrid, Hispania na pia ameonekana akifanya shughuli za ulinzi mwaka huu katika ziara za Houston, Boston na Umoja wa Mataifa.

Istanbul, Uturuki. Mmoja wa watuhumiwa aliyetambuliwa na maofisa wa Uturuki kuhusika katika tukio la kutoweka kwa mwandishi wa habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi ni ofisa ambaye amekuwa akiambatana mara kwa mara na Mwanamfalme Mohammed bin Salman.
Picha zimekuwa zikimwonyesha mtuhumiwa huyo akionekana akishuka kwenye ndege katika ziara za Salman jijini Paris, Ufaransa na Madrid, Hispania na pia ameonekana akifanya shughuli za ulinzi mwaka huu katika ziara za Houston, Boston na Umoja wa Mataifa.
Watuhumiwa wengine watatu wametajwa na mashuhuda na rekodi nyingine zilizoko kwa walinzi wa Mwanamfalme wa Saudi Arabia.
Mtuhumiwa wa tano ni daktari wa masuala ya upelelezi ambaye ana cheo cha juu katika Wizara ya Mambo ya Ndani na masuala ya tiba, ofisa wa kiwango hicho ambaye anaweza kutumwa tu na mamlaka za juu za Saudi Arabia.
Ikiwa, mamlaka za Uturuki zitasema, watu hawa walikuwepo katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul siku ya Oktoba 2 ambayo Khashoggi alitoweka basi mazingira hayo yataweka uhusiano wa nini kilitokea na Mwanaflame Salman.
Mazingira hayo yataondoa madai kwamba Khashoggi alikufa katika operesheni iliyofanywa na wahuni ambao wala hawakutumwa na mwanamfalme. Uhusiano huo unaweza kusababisha iwe vigumu kwa Ikulu ya White House na Baraza la Congress kukubali maelezo hayo.
Shirika la habari la New York Times limethibitisha kuwa walau watu tisa kati ya watuhumiwa 15 waliotambuliwa na mamlaka za Uturuki wamekuwa wakifanya kazi katika vitengo vya huduma za usalama, jeshi au wizara nyingine za serikali.
Mmoja wao, Maher Abdulaziz Mutreb, alikuwa mwanadiplomasia aliyekuwa katika ubalozi wa Saudia jijini London mwaka 2007, kwa mujibu wa orodha ya wanadiplomasia wa kigeni nchini Uingereza. Alikuwa akisafiri na mwanamfalme bila shaka kama mlinzi.