Mwanamke aliyeua wapenzi watatu kwa sumu kunyongwa

Muktasari:

  • Alitafuta wanaume kwa masharti kuwa wawe watu wazima, mwenye maradhi na matajiri.

Kyoto, Japan. Chisako Kakehi aliyebatizwa jina la ‘mwanamke muuaji’ huenda kesho akahukumiwa adhabu ya kifo kwa makosa ya kumuua mume wake na wapenzi wake wengine wawili kwa sumu ili arithi mali.

Kakehi (70) anatuhumiwa kuwaua wanaume hao kwa kuwawekea sumu aina ya sayanaidi (cyanide) baada ya kuandikishwa kuwa mrithi au kupata bima ya maisha ya wanaume hao matajiri.

Mwanamke huyo ambaye pia amebatizwa jina la black widow imebainika kuwa vifo vya wanaume hao vimemwachia utajiri wa pauni 6.85 milioni ambazo ni wastani wa Sh2.05 bilioni. Anatuhumiwa kutekeleza uhalifu huo kati ya mwaka 2007 na 2013.

Alikamatwa Novemba 2014 baada ya kifo cha mume wake Isao Kakehi ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu wafunge ndoa. Pia, anatuhumiwa kuwaua Masanori Honda na Minoru Hioki.

Katika mashtaka mengine anatuhumiwa kutaka kumuua rafiki yake Toshiaki Suero.

Mwanamke huyo amewahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume wengi lakini wote ni watu wazima na wenye kuugua maradhi.

Inaelezwa amekuwa akitafuta wapenzi kupitia mawakala lakini masharti yake siku zote yalikuwa ni lazima mwanamume awe mtu mzima, mwenye maradhi na utajiri.

Waendesha mashtaka wanasema wanaume wote walifariki baada tu ya kumuandika katika mirathi yao na kumuidhinisha katika bima ya maisha.