Polisi wadai hawakujua Kirumira kuwa hatarini

Friday September 14 2018

 

Kampala, Uganda. Jeshi la Polisi limesema halikuwa na habari zozote kwamba maisha ya aliyekuwa ofisa wake, hayati Muhammad Kirumira yalikuwa hatarini kabla ya tukio baya la kuuawa kwake Septemba 8 katika mji wa Bulenga, Wilaya ya Wakiso.
“Aliandikisha wapi malalamiko yake?” msemaji wa Polisi Emilian Kayima alisema akijibu swali aliloulizwa na gazeti la Daily Monitor lililotaka kujua kwa nini jeshi halikutaka kumlinda Kirumira.
Hivi sasa nyumba yake inalindwa na polisi kwa ushirikiano na jeshi.
Baba yake Kirumira, mzee Hajj Abubaker Kawooya, katika mahojiano  mapema wiki hii alihoji kwa nini chombo hicho cha ulinzi wa raia kilimwacha mtoto wake afe kivyake baada ya kutoa “taarifa nyeti” kuhusu magenge ya uhalifu yanayolindwa ndani ya polisi.
Baada ya kutoa taarifa nyeti kama hizo juu ya magenge ya uhalifu, polisi walipaswa kumpatia (Kirumira) ulinzi kama mmoja wa maofisa wake,” alisema Hajj Kawooya kisha akaongeza: “Na utaratibu kama huu unapaswa kuwa hivyo siyo kwa maofisa tu, bali jamii kwa ujumla hasa ambao wanafichua taarifa nyeti kuhusu shughuli za kihalifu”.
Polisi, katika majibu yao walisema ofisa, ambaye mara kadhaa amesambaza taarifa katika mitandao ya kijamii kuhusu kitisho dhidi ya maisha yake, hakuwahi kuandikisha malalamiko katika jeshi alilolitumikia.

Advertisement