Polisi waua waandamanaji wanaodai uhuru Cameroon

Muktasari:

  • Makundi yanayohamasisha wanaozungumza Kiingereza kujitenga na wenzao wanaozungumza Kifaransa yanaitwa Cameroon Action Group, Southern Cameroons Youth League, Southern Cameroons National Council, Southern Cameroon Peoples Organization na Ambazonia.

Polisi nchini wameua watu wanane na kuwajeruhi wengine wanane katika juhudi za kuwasaka wanaharakati waliokuwa wanahamasisha eneo hilo linalokaliwa zaidi na watu wanaozungumza Kiingereza kujitenga.

Wanaharakati waliandaa mgomo na maandamano yaliyolenga kujitangazia uhuru. Vikosi vya serikali vilitumwa kuzima jaribio la eneo hilo kujitenga.

Mwandamanaji mmoja aliuawa na askari alipojaribu kuinua bendera inayotarajiwa kuwa ya taifa hilo yenye rangi za bluu na nyeupe iliyobuniwa na kundi la Ambazonia.

Meya wa Kumbo, Donatus Njong Fonyuy ameliambia shirika la Reuters kuwa pia wafungwa walipigwa risasi na kufa baada ya moto kuzuka katika jela moja. Chanzo cha moto huo hakikujulikana.

Malalamiko ya watu kutoka eneo hilo lenye wakazi wanaozungumza Kiingereza ambazo ni asilimia 20 ya idadi ya watu, ni kubaguliwa katika mfumo wa elimu na sheria na kutopewa mgawo sawa kutokana na mapato yatokanayo na mafuta.

Madai ya kuwekwa kando yamekuwa malalamiko ya muda mrefu na kwamba vuguvugu la kujitenga lilianza kupata nguvu mwishoni mwa mwaka jana. Mgomo na maandamano ya Jumapili yalilenga kwenda sambamba na maadhimisho ya eneo hilo kupata uhuru kutoka Uingereza na kisha kuunga na wenzao wanaozungumza Kifaransa mwaka 1961.

Kundi moja lilitoa tangazo lililoashiria eneo hilo limepata uhuru wake Jumapili.

“Sisi si watumwa tena nchini Cameroon,” alisema Sisiku Ayuk, aliyejitambulisha kuwa rais wa Ambazonia.

“Leo tunathibitisha kuwa tuna mamlaka na eneo hili la urithi na ardhi yetu,” alisema kupitia mtandao wa kijamii.

Maandamano hayo pia yalitumika kama kigezo cha kupinga utawala wa Rais Paul Biya, ambaye amekaa madarakani kwa miaka 35. Biashara zilifungwa katika miji mikubwa ya eneo hilo ya Buea na Bamenda, huku helikopta zikiruka juu ya miji hiyo iliyohamwa na watu.

Mgogoro huo una historia ndefu kabla hata ya Vita ya Dunia I lakini viongozi wa sasa wanataka pamoja na mambo mengine kuheshimiwa katiba iliyokubaliwa mwaka 1961 katika Kongamano la Foumban inayotambua historia na utamaduni wa maeneo mawili hayo na kuyapa mamlaka maeneo yote mawili.

Rais Biya amelaani ghasia zilizotekelezwa na pande zote baada ya polisi kuwapiga risasi na kuwaua watu wanane na wengine wanane kujeruhiwa wakati wa maandamano hayo.