Shahidi mpya aeleza Habyarimana alivyouawa

Rais wa zamani wa Rwanda Juvenal Habyarimana

Muktasari:

Shahidi huyo mpya amezungumza na majaji hao walau mara mbili na anadai aliweka makombora mawili aina ya SA-16 kwenye gari katika makao makuu ya wapiganaji wa Rwandan Patriotic Front (RPF), Mulindi Machi 1994 yaliyopelekwa Kigali.

Paris, Ufaransa. Majaji wa mahakama moja nchini wamesikiliza, kutoka kwa shahidi mpya, madai kwamba aliona makombora yanayodaiwa kutumika kumuua Rais wa zamani wa Rwanda Juvenal Habyarimana ambaye kifo chache kilichochea mauaji ya kimbari mwaka 1994.

Kwa mujibu wa chanzo hicho ambacho kipo kiko karibu na kesi hiyo kimeliambia shirika la AFP kwamba shahidi huyo anasema aliona makombora hayo katika makao makuu ya wapiganaji wa kabila la Kitutsi wakiongozwa na Rais Paul Kagame ambayo baadaye ilitumika kuidungua ndege aliyokuwa amepanda Habyarimana.

Kombora hilo lililopigwa karibu na uwanja wa ndege mjini Kigali lilichochea vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumua kwa siku 100. Katika vita hivyo Watutsi waliouawa na Wahutu wa kabila la Habyarimana na inakadiriwa watu 800,000 walipoteza maisha.

Mahakama ya Ufaransa ambayo imechukua hatua ya kusikiliza malalamiko kutoka familia za raia wa Ufaransa waliouawa katika ndege hiyo aliyokuwa anasafiria Habyarimana waliamua Oktoba 2016 kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu mauaji hayo.

Jumla ya watu saba wamefunguliwa mashtaka wakidaiwa kuhusika na mauaji ya Wafaransa hao ambao ni pamoja na waziri wa sasa wa ulinzi James Kabarebe na mtu anayedaiwa kuitungua ndege hiyo, Franck Nziza.

Shahidi huyo mpya, ambaye amezungumza na majaji hao walau mara mbili, anadai aliweka makombora mawili aina ya SA-16 kwenye gari katika makao makuu ya wapiganaji wa Rwandan Patriotic Front (RPF), Mulindi Machi 1994 yaliyopelekwa Kigali.

Mtu huyo anayedaiwa kuandaa makombora "alituambia... kwamba walirusha makombora hayo kutoka eneo linaloitwa Massaka na hasa kutoka darajani ambako walikuwa na uwezo wa kuona vizuri uwanja wa ndege”.

Tofauti zaibuka

Hapa tayari kuna hoja mbili ambazo zinatofautiana. Kwa upande mmoja, inaarifiwa kuwa waasi wa zamani wa Rwanda wa Rwanda Patriotic Front (RPF) wakiongozwa na Paul Kagame, waliokuwa kwenye mlima wa Massaka walipewa agizo kudungua ndege ya Habyarimana.

Kwa upande mwingine, inaarifiwa kuwa makombora yalirushwa dhidi ya ndege ya rais Habyarimana kutoka kilomita 5 na kambi ya kijehi ya Kanombe iliyokua chini ya usimamizi wa jeshi la zamani la Rwanda (FAR), hapa ikimaanisha kuwa Wahutu wenye msimamo mkali walidungua ndege hiyo

Shahidi huyo mpya amesema kuwa alipewa majukumu ya kuhifadhi makombora mawili aina ya SA-16 katika makao makuu ya Waasi wa Kitutsi wa Rwanda wa RPF katika eneo la Mulindi. Shahidi huyo anadai kuwa alizungumza na Frank Nziza na Eric Hakizimana, ambao walirusha makombora hayo dhidi ya ndege ya Habyarimana.

Wote wanadai kuwa walirusha makombora hayo kutoka mlima wa Masaka, hali ambayo inahusisha kundi la zamani la waasi la RPF chini ya uongozi wa Paul Kagame. Shahidi huyo mpya, anasema Frank Nziza na Eric Hakizimana walimwambia kuwa makombora hayo yalirushwa akiwepo James Kabarebe. james kabarebe, ambaye ni Waziri wa Ulinzi wa Rwanda, na Frank Nziza wanachunguzwa tangu mwishoni mwa mwaka 2010.

Mahakama ya Ufaransa inataka kuwakutanisha kwa kuwasikiliza James Kabarebe, Frank Nziza na shahidi huyu mpya, katikati ya mwezi Desemba mwaka huu.

Bernard Maingain, mmoja wa wanasheria wa utawala wa Paul Kagame, amesema shahidi huyu mpya anakuja kuonyesha kutofautiana kwa mahakama ya Ufaransa.