Rais wa Catalonia aliyefutwa kazi akimbilia Ubelgiji

Muktasari:

  • Puigdemont ameondoka baada mwendesha mashtaka wa serikali kuu, Jose Manuel Maza kusema anafikiria kuandaa mashtaka ya uasi na uchochezi dhidi ya viongozi wa jimbo la Catalonia waliohusika katika mchakato wa kujitangazia uhuru.

Barcelona, Catalonia. Rais wa Catalonia aliyeondolewa madarakani Carles Puigdemont amekimbilia Ubelgiji, wakili wake Paul Bekaert amesema.

Bekaert aliyeko Ubelgiji hakusema ikiwa Puigdemont anakusudia kuomba hifadhi ya kisiasa au la lakini Waziri anayeshughulikia hifadhi ya wakimbizi wa kisiasa na wahamiaji wa Ubelgiji Theo Francken amesema huenda rais huyo wa zamani akaomba hifadhi.

Vyombo vya habari vya Hispania vimeripoti kwamba Puigdemont ameongozana na maofisa wa iliyokuwa serikali ya Catalonia ambao idadi yao haijajulikana. Msafara wa kiongozi huyo na Francken unatarajiwa kutoa taarifa ya pamoja leo.

Puigdemont ameondoka baada mwendesha mashtaka wa serikali kuu, Jose Manuel Maza kusema anafikiria kuandaa mashtaka ya uasi na uchochezi dhidi ya viongozi wa jimbo la Catalonia waliohusika katika mchakato wa kujitangazia uhuru.

Maza alisema anafikiria kuwashtaki viongozi waandamizi akiwemo rais huyo aliyeondolewa na baraza lake la mawaziri baada ya bunge kupiga kura kuidhinisha tangazo la kujitangazia uhuru wiki iliyopita.

Huu ni mwendelezo mpya baada ya serikali kuu kuamua Jumatatu kuchukua udhibiti wa Catalonia na kuiongoza moja kwa moja kutoka Madrid. Mbali ya kuongoza moja kwa moja pia ilivunja bunge na imeitisha uchaguzi mpya Desemba 21.

Mzozo kati ya Catalonia na Hispania ni wa muda mrefu lakini ulizidi kuwa mbaya baada ya Puigdemont kusimamia eneo hilo moja ya majimbo yenye utawala wa ndani, kupiga kura ya maoni Oktoba Mosi kuamua kuwa huru jambo ambalo ni kinyume cha Katiba ya Umoja ya Hispania na kinyume cha amri ya mahakama iliyopiga marufuku.

Catalonia walipiga kura ambapo imeelezwa walioshiriki walikuwa asilimia 43 ya wapigakura halali na kati yao asilimia 90 waliunga mkono eneo hilo kujitangazia uhuru. Ijumaa iliyopita Bunge la Catalonia lilipiga kura kuridhia kujitenga lakini siku hiyo hiyo serikali kuu ilitumia kifungu cha 155 cha Katiba kuifuta serikali ya Catalonia na kuweka utawala wa muda.