Al-Shabab wakata vichwa watu saba Msumbiji

Muktasari:

  • Wahalifu walitumia mapanga kuua watu saba. Tunafikiri kikundi hiki ni sehemu ya kile kilichoua watu 10 kwa kukata vichwa Mei 27," msemaji wa polisi Inacio Dina aliliambia shirika la AFP akirejea shambulizi la mwezi uliopita katika jimbo hilo.

Maputo, Msumbiji. Washambuliaji kadhaa Jumanne waliua watu saba kwa kukata vichwa vyao kwa mapanga na kuchoma nyumba zaidi ya 10 Kaskazini mwa nchi, eneo ambalo lilikumbwa na shambulizi kama hilo hivi karibuni.
Jimbo la Cabo Delgado, ambalo linatarajiwa kugeuka kuwa makao makuu ya uzalishaji gesi asilia baada ya ugunduzi wa hivi karibuni kuonyesha matumaini, limekuwa likishuhudia mashambulizi ya mauaji dhidi ya vikosi vya usalama na raia tangu Oktoba mwaka jana.
"Wahalifu walitumia mapanga kuua watu saba. Tunafikiri kikundi hiki ni sehemu ya kile kilichoua watu 10 kwa kukata vichwa Mei 27," msemaji wa polisi Inacio Dina aliliambia shirika la AFP akirejea shambulizi la mwezi uliopita katika jimbo hilo.
"Washambuliaji, Jumanne alfajiri, walichoma moto nyumba 164 na waliharibu magari manne walipofanya shambulizi katika kijiji cha Naude wilaya ya Macomia," alisema.
Washambuliaji ambao wenyeji na maofisa wanadai kuwa ni "al-Shabab", hawana uhusiano wowote na wale wa Somalia wanaotumia silaha na jina hilo hilo.
Baada ya tukio la awali polisi waliongezwa katika eneo hilo kuimarisha usalama.
Dina alidokeza kuwa kikundi hicho kinaweza kuwa na uhusiano na “waasi” tisa waliouawa na vikosi vya usalama mwishoni mwa wiki waliogundulika kuwa na bunduki za kivita na nyaraka zilizoandikwa kwa Kiarabu.
"Kundi hili limegawanyika sana katika vikundi vidogo ambavyo vinajaribu kukabiliana na vishindo vya mashambulizi ya polisi,” alisema.