Saudi Arabia kufafanua mwandishi alivyofia ubalozini

Muktasari:

  • Chanzo kimoja kimesema ripoti hiyo itahitimisha kwamba operesheni hiyo ilifanyika bila kibali na uwazi na kwamba wale waliohusika watawajibishwa.
  • Chanzo kingine kimekiri kwamba ripoti bado inaandaliwa na kilionya kwamba mambo yanaweza kubadilika.
  • Mpenzi wa Khashoggi, Hatice Cengiz, ambaye alikuwa akimsubiri nje ya ubalozi, anasema hakumwona tena akitoka nje.

Ankara, Uturuki. Saudi Arabia inaandaa ripoti ambayo itakubali kuwa kifo cha mwandishi wa habari Jamal Khashoggi kilitokana na mahojiano ambayo yalikwenda mrama, ambayo yalitarajiwa kuwaongoza kumteka kutoka Uturuki, kwa mujibu wa vyanzo viwili.
Chanzo kimoja kimesema ripoti hiyo itahitimisha kwamba operesheni hiyo ilifanyika bila kibali na uwazi na kwamba wale waliohusika watawajibishwa.
Chanzo kingine kimekiri kwamba ripoti bado inaandaliwa na kilionya kwamba mambo yanaweza kubadilika.
Khashoggi, ambaye alikuwa mwandishi wa safu katika gazeti la The Washington Post alionekana kwa mara ya mwisho akiingia kwenye jingo la ubalozi mdogo wa Saudi Arabia uliopo Istanbul, Uturuki Oktoba 2. Awali, mamlaka za Saudi Arabia ziling’ang’ana kwamba Khashoggi aliondoka mchana siku ileile lakini haikutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai hayo.
Mpenzi wa Khashoggi, Hatice Cengiz, ambaye alikuwa akimsubiri nje ya ubalozi, anasema hakumwona tena akitoka nje.
Kutoweka kwake kuliibua mgogoro wa kidiplomasia kati ya Saudi Arabia na mataifa ya Magharibi. Katikati ya mzozo huo, makampuni ya kimataifa yalianza kujiondoa kushiriki mkutano wa ngazi ya juu wa uwekezaji, kongamano la Mpango wa Baadaye wa Uwekezaji unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao Riyadh.
Suala hilo lilisababisha msuguano kati ya Saudi Arabia na Uturuki, ambayo mara kwa mara ilikuwa ikiishutumu Saudi Arabia kwa kushindwa kushirikiana na wapelelezi wake.
Mamlaka za Uturuki hapo awali zilisema zilikuwa zinaamini kwamba maofisa wapatao 15 kutoka Saudi Arabia waliingia Istanbul Oktoba 2 na ndio wanahusishwa na kutoweka kwa Khashoggi na uwezekano wa kuuawa kwake. Angalau baadhi yao wanaonekana kuwa na uhusiano wa kiwango cha juu katika serikali ya Saudi.