Tume yaanika mpango wa kuzuia ulaghai wa kura

Muktasari:

 

  • Wasimamizi hawataruhusiwa kutuma matokeo bila kuambatanisha uthibitisho wa fomu zilizotiwa saini.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeweka wazi utaratibu mpya wa kudhibiti ulaghai katika uchaguzi wa marudio Oktoba 26 ambapo sasa maofisa wasimamizi hawataruhusiwa kutuma matokeo bila kuambatanisha uthibitisho wa fomu zilizotiwa saini.

Mkakati huo wa kudhibiti ulaghai umebainishwa katika mkataba ulioingiwa kati ya IEBC na kampuni ya vifaa vya usalama ya OT-Morpho kutoka Ufaransa. Katika mkataba huo wenye thamani ya Sh2.4 bilioni, Tume inataka kuziba mianya yote iliyochangia kufutwa na Mahakama ya Juu matokeo yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 8.

Ikiwa mapendekezo yote yatatekelezwa kikamilifu, maofisa wote wasimamizi wa uchaguzi vituoni na kwenye majimbo watatakiwa kutuma njia ya mfumo wa elektroniki fomu za matokeo zilizotiwa saini kwenye kituo cha kujumlishia badala ya meseji zilizotumika katika uchaguzi uliofutwa.

Kampuni hiyo kutoka Ufaransa, ambayo imeiuzia IEBC vifaa vya mawasiliano ya kiteknolojia imeajiri watu 400 kusambaza vifaa hivyo na kujenga na atakuwepo injinia mmoja katika kila jimbo siku ya uchaguzi.

Viongozi wa OT-Morpho, wakiridhia ombi la IEBC wamesema kwamba “utendaji wa mfumo mpya wa utumaji matokeo utawawezesha maofisa wasimamizi wa IEBC kupata fomu rasmi Fomu 34B zilizojazwa, kuhakikiwa na kutiwa saini na IEBC”.