Wanajeshi waliomng’oa rais wapewa tuzo

Muktasari:

  • Sheria hiyo inampa Rais Abdel Fattah al-Sisi haki ya kuwateua maofisa ambao wanastahili tuzo ambayo ni pamoja na zawadi mbalimbali kutokana na jitihada zao hizo.

Cairo, Misri. Bunge la Misri limepitisha sheria ambayo inaweza kuwafanya maofisa waandamizi wa jeshi kuwa na kinga kuhusiana na ghasia ambazo zilisababisha kung’olewa Rais Mohamed Morsi mwaka 2013.

Sheria hiyo inampa Rais Abdel Fattah al-Sisi haki ya kuwateua maofisa ambao wanastahili tuzo ambayo ni pamoja na zawadi mbalimbali kutokana na jitihada zao hizo.

Pia inawapa kinga dhidi ya uchunguzi wa makosa yoyote yaliyofanywa kuanzia Julai 3, 2013 hadi Juni 8, 2014 katika kipindi ambacho Morsi aliondolewa madarakani hadi katika siku ya mwanzo ya al-Sisi kuwa rais.

Watu wengi waliuawa wakati majeshi ya usalama yalipovunja kwa nguvu maandamano ya kukalia eneo la Uwanja wa Rabaa mjini Cairo wakimuunga mkono Mursi Agosti 2013, katika mojawapo wa matukio yaliyomwaga damu kwenye historia ya Misri.

Akihutubia kwa njia ya televisheni mara baada ya mapinduzi hayo, al-Sisi aliyekuwa mkuu wa majeshi alisema katiba ya Misri imesitishwa kwa muda na mkuu wa mahakama ya katiba kuteuliwa kuwa kiongozi wa muda nchini.

Al-Sisi alitangaza kwamba jeshi lilikuwa linaangalia masilahi ya watu wa Misri baada ya maandamano makubwa ya upinzani yaliyomtaka Rais Morsi kujiuzulu.

Kufuatia hotuba yake hiyo katika televisheni, Morsi alitoa taarifa kupitia akaunti yake ya Twitter, akiita hatua ya jeshi ni “mapinduzi kamili”. Pia aliwasihi Wamisri wote kukataa hatua hiyo ya jeshi na kuwataka kuwa na amani.

Kama sehemu ya mwongozo mpya ulioungwa mkono na jeshi, al sisi alitaka uwepo uchaguzi wa rais na wabunge pamoja na jopo kutathmini katiba na kamati ya mashauriano kitaifa. Alisema mwongozo ulikubaliwa na makundi kadhaa ya kisiasa na pia kuwasihi watu wa Misri kuacha vurugu.

Jeshi lilimpa Morsi saa 48 kutatua matatizo ya kisiasa au kuwepo hatari ya jeshi kuingilia kati.

Morsi ni nani?

Morsi ni mwanasiasa wa Misri na rais wa tano wa Taifa hilo aliyetawala kuanzia Juni 30, 2012 hadi Julai 3, 2013 alipopinduliwa na al-Sisi kufuatia maandamano makubwa ya kupinga utawala wake.

Kiongozi huyo alikuwa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia katika historia ya Taifa hilo baada ya miaka mingi ya utawala usio na uchaguzi.

Morsi ni msomi aliyefikia ngazi ya PhD na alikuwa mwanachama mwandamizi wa kundi la Udugu wa Kiislamu. Awali, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa tawi la kisiasa la Chama cha Haki na Uhuru (FJP), kilichoundwa na Udugu wa Kiislamu baada ya mapinduzi ya mwaka 2012.