Kimbunga cha Mangula chatimua watumishi wa umma walioshinda CCM

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), George Mkuchika akisisitiza jambo kwenye mkutano na  waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Suzan Mlawi. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Mkuchika, ambaye ni waziri mpya wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, alisema jana kuwa suala hilo linatakiwa litekelezwe kulingana na mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi.

Morogoro. Sakata la watumishi wa umma kugombea uongozi ndani ya CCM limeendelea kutikisa baada ya chama hicho mkoani Morogoro kumuondoa aliyeshinda uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, huku Waziri George Mkuchika akisema watalishughulikia kwa mujibu wa taratibu.

Mkuchika, ambaye ni waziri mpya wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, alisema jana kuwa suala hilo linatakiwa litekelezwe kulingana na mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi.

Alisema wakati nchi inaingia kwenye mfumo wa vyama vingi, Katibu Mkuu Kiongozi alitoa mwongozo ambao ulielekeza watumishi wa umma kutojihusisha na uongozi wa vyama vya siasa, isipokuwa baadhi.

Mwongozo huo pia ulizuiwa watumishi wa umma kuendesha shughuli za siasa katika ofisi na majengo ya umma.

Lakini katika uchaguzi wa viongozi wa wilaya, baadhi ya watumishi wa umma waligombea nafasi mbalimbali na baadhi yao kushinda, akiwemo Salvatory Richard, ambaye ni mtumishi wa Idara ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.

Richard alishinda nafasi ya mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi katika uchaguzi uliofanyika Septemba 23 wilayani Mvomero baada ya kupata kura 226 na kumbwaga mpinzani wake, Dominick Elisha aliyepata kura 138.

Baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo Elisha alikata rufaa akilalamika kuwa mshindi wa nafasi ya uenyekiti ni mtumishi wa Serikali na kuhoji uhalali wa kushiriki uchaguzi wa chama.

Hata baada ya rufaa hiyo uongozi wa Wazazi uliendelea kuwa kimya hadi makamu mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula alipoagiza watumishi wote wa umma kuchagua siasa ama ajira, ndipo uongozi wa mkoa ulipoamua kutangaza kurudia uchaguzi wa nafasi hiyo.

Baada ya uchaguzi huo, katibu tawala wa Morogoro, Clifford Tandari alinukuliwa akiagiza watumishi wote wa umma walioshinda nafasi za kisiasa kuchagua moja, kati ya siasa na ajira.

Sheria Namba 8 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002, Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za 2009 zinamtaka mtumishi aliyechaguliwa katika nafasi za kisiasa kuacha kazi na kutumikia nafasi yake ya kisiasa.

Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Namba 1 wa mwaka 2015 kuhusu utaratibu wa watumishi wa umma wanaogombea nyadhifa za kisiasa nchini umeweka wazi kuwa atakayeamua kugombea nafasi ya siasa atalazimika kuacha kazi.

Kipengele cha 3:1:6 cha waraka huo kinasema, “mtumishi wa umma atakayeamua kugombea nafasi yoyote katika chama cha siasa atalazimika kuacha kazi na kulipwa mafao yake”.

Kipengele 7:1 cha waraka huo kinaeleza endapo mtumishi atashindwa na akataka kurejea kazini, hana budi kuomba kazi upya kwenye mamlaka husika.

Akizungumzia hatua hiyo, Katibu wa Wazazi wa CCM mkoani Morogoro, Selemani Pinde alisema kilichomuondoa mtumishi huyo ni Waraka wa Utumishi wa Umma unaomzuia kugombea nafasi za kisiasa na si CCM.

“Chama chetu ni cha wakulima na wafanyakazi hivyo sisi kama chama hatuwezi kumzuia mtumishi kugombea, ila anachotakiwa ni kujipima kama ataacha utumishi ili atumikie chama kwa kuwa upande wa utumishi unambana kutumikia nafasi mbili,” alisema katibu huyo.

Pinde alisema tayari wameshatangaza kurudia uchaguzi huo na fomu zimeshaanza kutolewa tangu Oktoba 15, na tayari watu watano wameshachukua fomu na uchukuaji fomu utamalizika leo saa 10:00 jioni.

Aliwataja waliochukua fomu na kata wanazotoka kuwa ni Dominick Elisha (Dihongoya), Majuka Koila (Mkindo), Paschal John (Mtibwa), Winfrida Mzeru (Dihongoya) na Oswald Mlay (Mtibwa).

Katika uchaguzi huo, wakuu wa wilaya waligombea nafasi za ujumbe wa mkutano mkuu wa CCM na baadhi kushinda. Baadhi ya walioshinda ni Simon Odunga (Chemba), Christina Mndeme (Dodoma) na Elizabeth Kitundu (Bai) mkoani Dodoma.

Wengine ni Alhaji Mohamed Utaly (Mvomero), Seriel Nchembe (Gairo), Alexander Mnyeti (Arumeru), Raymond Mushi (Babati, Manyara) na Herman Kapufi (Geita).

Pia yumo Kaul Kiteleki, ambaye ni katibu tarafa wa Makuyuni (Arusha), Salum Palango (katibu tawala wa Nanyumbu, Elishilia Kaaya ambaye ni mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) na Dk Daniel Mrisho.