King Long yaingiza mabasi yake nchini

Muktasari:

Uzinduzi wa usambazaji wa mabasi hayo ulifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Serikali ya China kupitia Kampuni ya King Long imeanza rasmi kuingiza nchini mabasi yake.

Uzinduzi wa usambazaji wa mabasi hayo ulifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Dar es Salaam.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja Masoko wa King Long, Kanda ya Kusini mwa Afrika, Danny Fu alisema wameamua kuingia nchini baada ya kukamilisha utafiti wa kubaini njia bora ya kutengeneza mabasi.

Alisema Kampuni ya King Long ilianza kutengeneza mabasi mwaka 1988 na kuyasambaza nchi za Mashariki ya Kati, Ulaya, Australia na New Zealand kabla ya kuja Afrika Mashariki.

Fu alisema tofauti na kampuni nyingine za kutengeneza mabasi, kampuni hiyo baada ya kumuuzia mteja inaendelea kuwa na uhusiano naye kwa ajili ya kutoa msaada wa kiufundi na kurahisisha upatikanaji wa vipuri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Pwani Motors Ltd, Abdul Virjee alitoa wito kwa wafanyabiashara kununua mabasi hayo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Tawakal, Nabil Tawakal alisema umefika wakati kwa wafanyabiashara kuangalia kampuni zinazotengeneza mabasi bora ya biashara ili kuepuka hasara za mara kwa mara zinazosababishwa kutokuwa imara.

“Nilinunua mabasi mawili ya King Long hayakunisumbua, nimeongeza mawili na naona yananitendea haki,” alisema Tawakal.

Mmiliki wa Kampuni ya Happy Nation, Issa Nkya alitoa wito kwa kampuni hiyo kuongeza ukubwa wa tangi la kuhifadhi mafuta ili kumudu safari ndefu.

Nkya ambaye aliagiza mabasi mapya 12 katika hafla hiyo, alisema matangi yanapaswa kuwa na uwezo wa kuhifadhi hadi lita 800 za dizeli.

Kuingia rasmi nchini kwa kampuni hiyo ya kutengeneza mabasi, kunafanya idadi ya kampuni za kutengeneza mabasi kutoka China kufikia tano.