Kinondoni, Siha zilivyoipa wakati mgumu Chadema

Mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya CUF, Rajab Salim Juma akipunga mkono alipokuwa akienda katika ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo jijini Dar es Salaam. Picha na Salim Shao

Muktasari:

  • Ugumu huo unatokana na uongozi wa ngazi ya jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro kumaliza mchakato wa kura ya maoni na kuwapata wagombea, hivyo kusubiri baraka za Kamati Kuu ya chama hicho ilichofanyika jana.

 Majimbo ya Kinondoni na Siha yameiweka katika wakati mgumu Chadema kuamua iwapo itashiriki uchaguzi mdogo au itaendelea kususia kama ilivyofanya katika uchaguzi mdogo wa Janauri 13.

Ugumu huo unatokana na uongozi wa ngazi ya jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro kumaliza mchakato wa kura ya maoni na kuwapata wagombea, hivyo kusubiri baraka za Kamati Kuu ya chama hicho ilichofanyika jana.

Kukamilika kwa mchakato huo kunaifanya Kamati Kuu ya Chadema kuwa katika wakati mgumu wa kuamua ama chama hicho kishiriki katika uchaguzi huo mdogo wa Februari 17 au kiendelea na msimamo wa kutokushiriki hadi kile wanachokilalamikia kipate ufumbuzi.

Chadema pamoja na vyama vinavyounda Ukawa vya NLD, CUF na NCCR-Mageuzi na vyama vingine vya Chauma na ACT- Wazalendo vilisusia uchaguzi huo kwa kile kilichoelezwa kutokuridhishwa na mazingira ya uchaguzi wa udiwani katika kata 43 uliofanyika Novemba 26, mwaka jana.

Vyama hivyo viliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusitisha uchaguzi huo ili kutoka fursa ya kukutana nayo kufanya tathimini ya mazingira ya uchaguzi huo jambo ambalo hata hivyo NEC ililipinga ikisema inasimami sheria na vyama hivyo pia havikushiriki katika uchaguzi uliohusisha majimbo matatu ya Singida Kaskazini, Songea Mjini na Longido.

Baada ya uongozi wa jimbo wa Kinondoni na Siha kumaliza mchakato, jana kikao cha dharura cha Kamati Kuu kilikutana jijini Dar es Salaam ambacho kinaeleza pamoja na mambo mengine suala hilo la kuamua kushiriki au kutokushiriki lilijadiliwa.

Baadhi ya viongozi na wabunge wa Chadema wanaona kuna kila sababu ya kushiriki uchaguzi huo mdogo kwani uwezekano wa kushinda wanaouna ni mkubwa hasa ikizingatiwa uamuzi wa CCM kuwapitisha wagombea walewale waliokuwa wabunge katika maeneo hayo.

Kinondoni wamempitisha Maulid Mtulia aliyekuwa mbunge kupitia CUF na Dk Godwin Mollea aliyekuwa Chadema ambao wote walitangaza kuhamia CCM katika jitihada za kumuunga mkono Rais John Magufuli.

Hoja nyingine inayoiweka Chadema katika wakati mgumu ni mazingira ya majimbo hayo hususan la Kinondoni kwamba wanaweza kuweka mawakala katika kila kituo pamoja na kuwa Jiji la Dar es Salaam kitovu cha nchi huku leo ikiwa ni siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu ya kugombea ubunge.

Pia inajitokeza hoja ya Chadema kuamua peke yake kushiriki, wakati uamuzi wa kususia uchaguzi huo iliupitisha kwa kushirikiana na vyama vinavyounda Ukawa.

Msemaji wa Chadema, Tumain Makene alithibitisha kuwapo kwa kikao hicho cha Kamati Kuu huku akishindwa kueleza agenda ni zipi na ni cha siku ngapi.

Juzi, kamati ya utendaji ya wilaya ya Siha ilifanya uteuzi wa awali na kumteua Elvis Mossi kugombea ubunge jimbo la Siha.

Katibu wa Chadema mkoa Kilimanjaro, Basil Lema, alisema uteuzi huo wa Mossi utasubiri baraka za Kamati Kuu ya Chadema.

“Kilichofanyika ni uteuzi tu wa awali kamati kuu ikishatoa hilo jina ndio inakuwa rasmi. Kamati kuu ina mamlaka ya kukubali, kukataa au hata kubadilisha mgombea,” alisema katibu huyo. Wakati hayo yakiendelea kwa vyama hivyo, CUF upande wa Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba jana ilimsindikiza mgombea wake wa jimbo la Kinondoni, Rajabu Salim Juma kuchukua fomu katika ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni.

Vyama vingine ambavyo vitasimamisha wagombea na wameshachukua fomu ni CCM, Sau, Demokrasia Makini, TLP, UMD na DP.

Imeandikwa na Ibrahim Yamola, Raymond Kaminyonge (Dar) na Daniel Mjema (Kilimanjaro)