Thursday, December 7, 2017

Viongozi wa Serikali Arusha wanyooshewa kidole

 

By Moses Mashalla, Mwananchi mmashalla@mwananchi.co.tz

Arusha. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Loota Sanare amewanyooshea vidole baadhi ya viongozi wa Serikali mkoani hapa kwamba walitaka kuingilia uchaguzi ndani ya chama hicho na kudiriki kupanga safu zao.

Amesema katika uongozi wake, hatapenda kuona mambo hayo yakiendelea katika chaguzi zijazo, akiwashauri viongozi wa Serikali kumsaidia Rais John Magufuli kutekeleza ilani ya CCM.

Sanare bila kutaja majina ya viongozi hao, amesema Serikali inapaswa kuacha kuingilia uchaguzi wa CCM ili wanachama wachague watu wanaowataka.

“Tumeingiliwa, watu wanataka kutuchagulia viongozi wa CCM, viongozi wetu wa Serikali ndani ya mkoa na wilaya tunapofanya uchaguzi ndani ya chama watuachie tuwachague tunaowataka,” amesema Sanare.

Msimamizi wa uchaguzi, Stephen Wasira akitangaza matokeo jana Jumatano Desemba 6,2017 usiku, alimtangaza Sanare mshindi wa uenyekiti wa mkoa kwa kura 454 dhidi ya Lekule Laiser aliyepata kura 352 na Juma Losini aliyepata kura 12.

Wasira aliwataka wanachama kuwa kitu kimoja na kufanya kazi bila makundi ili kuepusha  migogoro ya mara kwa mara inayojitokeza mkoani Arusha.

Laiser aliwashukuru wajumbe waliompigia kura akisema ni lazima wajifunze kukubaliana na matokeo ili kuepusha makundi baada ya uchaguzi.

Wajumbe walimchagua Daniel Awakii kutoka wilayani Karatu kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Shaaban Mdoe ambaye ni mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru kuwa katibu wa uenezi wa mkoa.

-->