Kiongozi Chadema avuruga mkutano CCM, apokea kichapo

Muktasari:

Kiongozi huyo wa Chadema alituhumiwa na wanachama na wafuasi wa CCM kuvuruga mkutano wao wa kampeni ya uchaguzi mdogo Kata ya Kahumulo wilayani humo jana baada ya kupita jirani na eneo la mkutano akitangaza mkutano wa chama chake kupitia vipaza sauti na hivyo kuvuruga usikivu.

Sengerema. Katibu Chadema jimbo la Sengerema, Deusdeth Mwigala  alionja joto ya jiwe baada ya kushambuliwa kwa kipigo hadi kupoteza fahamu na wafuasi waliodaiwa  kuwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa tuhuma za kuvuruga mkutano wa chama hicho.

Kiongozi huyo wa Chadema alituhumiwa na wanachama na wafuasi wa CCM kuvuruga mkutano wao wa kampeni ya uchaguzi mdogo Kata ya Kahumulo wilayani humo jana baada ya kupita jirani na eneo la mkutano akitangaza mkutano wa chama chake kupitia vipaza sauti na hivyo kuvuruga usikivu.

Hata hivyo, Katibu huyo alikana tuhuma za kuvuruga mkutano wa CCM akidai alikuwa umbali wa zaidi ya mita 200 kutoka eneo lilipokuwa mkutano wa CCM.

“Nikiwa naendelea na kazi ya kutangaza mkutano wa Chadema nikiwa nimeongozana na makada wengine wanne pamoja na dereva, ghafla tulivamiwa na watu wa CCM na kuanza kutushambulia,” amesema Mwigala

Katibu wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), Wilaya ya Sengerema Hasan Moshi amesema  vijana wa chama hicho walihamaki na kumwadhibu kiongozi huyo wa Chadema baada ya kuvuruga mkutano wao makusudi kwa kutoa matangazo yanayoingilia mkutano uliokuwa unaendelea.