Kiongozi wa Mwenge apinga masharti mikopo ya pikipiki

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Charles Kabeho

Muktasari:

  • Amesema anapata tabu kuuelewa utaratibu huo kwa sababu mtumishi wa umma anapokopeshwa chombo cha usafiri na kukatwa mshahara huwa mali yake binafsi.

Chalinze. Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Charles Kabeho amesema haiingii akilini pikipiki wanazokopeshwa maofisa ugani ambao hukatwa sehemu ya mishahara yao zitumike kwa shughuli za kiserikali pekee.

Amesema anapata tabu kuuelewa utaratibu huo kwa sababu mtumishi wa umma anapokopeshwa chombo cha usafiri na kukatwa mshahara huwa mali yake binafsi.

Kabeho alisema hayo mwishoni mwa wiki katika Kijiji cha Mazizi ambako pikipiki 15 zilikabidhiwa kwa maofisa ugani wa kata 15 za Halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani.

Pikipiki hizo zimegharimu Sh34 milioni na maofisa hao watapaswa kulipia Sh18,700 kila mwezi kwa kipindi cha miaka mitano.

Kabeho alisema hata kama halmashauri imepanga kuwapatia mafuta kila wiki, hilo halibadilishi utaratibu unaotumika kukopesha pikipiki hizo.

Awali, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Edes Lukoa alisema uamuzi wa kuwakopesha pikipiki ulipitishwa na baraza la madiwani baada ya kuona watumishi wengi wakiwamo maofisa ugani wanapata tabu kufika maeneo ya kazi vijijini.

Lukoa alisema halmashauri hutumia fedha za mapato ya ndani kununua pikipiki na watumishi hurejesha fedha kila mwezi kwa miaka mitano.

Kabeho aliishauri halmashauri hiyo kubadili mkataba wa ukopeshaji pikipiki hizo ili zitolewe kwa ajili ya kazi na ikitokea mtumishi amehama aiache.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga aliahidi kusimamia ubadilishwaji wa mkataba ili isiwe mkopo, bali zitabaki chini ya ofisi za kata kwa ajili ya shughuli za maofisa ugani vijijini.