Kipilimba wa NIDA ateuliwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa

Rais John Magufuli akimuapisha Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Dk Modestus Kipilimba leo Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na Ikulu

Muktasari:

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Ikulu imeeleza kuwa kabla ya uteuzi huo Dk Kipilimba alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli amemteua Modestus Francis Kipilimba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Ikulu imeeleza kuwa kabla ya uteuzi huo Dk Kipilimba alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Pia Dk Kipilimba amewahi kuwa Mkurugenzi wa Daftari la Kudumu na Tehama wa  Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Dk Kipilimba anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Rashid Othman ambaye amestaafu.

Dkt. Modestus Francis Kipilimba ataapishwa leo mchana tarehe 24 Agosti, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Wakati huo huo Rais Magufuli amemteua Robert Msalika kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Kabla ya uteuzi huo   Msalika alikuwa Afisa Ubalozi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia.

Kadhalika Rais  Magufuli amemteua aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa George Madafa kuwa Balozi na nchi atakayopangiwa itatajwa baadaye.

Wakurugenzi na Naibu Wakurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa waliopo wanaendelea na nafasi zao.