Kishindo cha Nape Dar es Salaam

Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Hotuba hiyo aliitoa akiwa amesimama juu ya gari mithili ya mwanasiasa aliyesimamishwa na wananchi ili azungumze nao baada ya uongozi wa Hoteli ya Protea kuamriwa usiruhusu kufanyika kwa mkutano wake na waandishi wa habari.

Dar es Salaam. Saa chache baada ya kuvuliwa uwaziri. Nape Nnauye ameacha kishindo baada ya juhudi za kuzuia mkutano wake kushindikana, kukabiliana na askari kanzu waliomtishia kwa bastola, na baadaye kutoa hotuba.

Hotuba hiyo aliitoa akiwa amesimama juu ya gari mithili ya mwanasiasa aliyesimamishwa na wananchi ili azungumze nao baada ya uongozi wa Hoteli ya Protea kuamriwa usiruhusu kufanyika kwa mkutano wake na waandishi wa habari.

Nape alikuwa amepanga kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu kuvuliwa uwaziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo uliofanywa na Rais Magufuli jana asubuhi.

Mara baada ya kufika Protea iliyopo Oysterbay karibu na Kanisa la St. Peters, Nape alishuka kwenye gari lake lililokuwa na namba za Serikali na kuanza kuelekea majengo ya hoteli hiyo.

Ghafla akatokea kijana mmoja aliyevalia shati jeupe na suruali ya jeans huku kiunoni ikionekana bastola iliyochomekewa kwa nyuma. Kijana huyo alionekana akibishana na Nape na muda mfupi baadaye kijana mwingine aliyevalia fulana ya bluu yenye mistari myeupe na suruali ya jeans akaongeza nguvu.

Lakini Nape alionekana kutokubaliana na amri yao na ndipo kijana aliyevalia fulana aliporudi nyuma na kuchomoa bastola akimnyooshea Nape, kabla ya kumsogelea tena.

Wakati akifanya hivyo, kijana mwingine aliyevalia suti ya bluu alimuendea Nape kwa nyuma akafungua mlango wa gari na baadaye kumvuta mkono, huku wengine wawili wakimsukuma kuelekea kwenye gari na ndipo mbunge huyo wa Mtama alipoonekana kuzidiwa nguvu. Walipomfikisha mlangoni lilitokea gari jingine lililosogea karibu na kusimama kwa muda mfupi na baadaye kuondoka.

Wakati Nape akionekana kuzidiwa nguvu, kijana mmoja alienda hadi mlangoni mwa gari la Nape na kumuondoa askari kanzu huyo na wakati waandishi wa habari wakizidi kujongea karibu kupata tukio hilo vizuri, vijana wawili waliosalia waliondoka.

Baadaye waandishi walimtaka Nape azungumze alichotaka kusema na ndipo alipopanda juu ya gari kuzungumza.

“Nataka waliokuja kuzuia mkutano wawaambie kwa nini wanazuia mkutano,” alisema Nape akiwaambia waandishi wa habari nje ya hoteli hiyo huku wapita njia wakizidi kuongezeka eneo hilo.

“Wanatoa bunduki hadharani, wanataka nifanye ambayo sikuwaza kufanya. Wanataka kuniua. Msiwe na hofu. Nataka waliotoa bunduki kwenye hii shughuli waseme nani aliwatuma kuzuia huu mkutano. Nataka hili kabla ya kuingia kwenye gari na kuondoka.

“Tusifanyiane mambo ya kijinga. Nchi huru hii. Mimi ni mwanahabari, nisipopigania uhuru wa hawa wanahabari napigania uhuru wa nani.

“Wamesahau wakati mimi nalala porini wao kule walikuwa wanakunywa bia baa.”

Nape alisema alidhani mkutano wake na waandishi ungekuwa wa amani kwa sababu nia yake haikuwa mbaya kwa Serikali na chama chake.

“Nia yangu ilikuwa ni kuwaeleza Watanzania kuwa maisha lazima yaendelee. Sasa wanapokuja wapuuzi wachache na wanadhani wanaweza kukoroga hivi mambo, nataka vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi hii viangalie wanachokifanya,” alisema Nape.

“Mimi niliteuliwa. Sikuulizwa wakati ninateuliwa, kwa hivyo wakati anataka kuweka mtu mwingine, sina sababu ya kuuliza na wala sina kinyongo na Rais wangu. Sijasema chochote kama nina kinyongo. Kwa nini kuna watu wanataka kufika mahali wao ndiyo waamuzi wa mawazo ya vijana wa nchi hii?”

Nape alisema vijana lazima wasikie alichotaka kusema.

“We have nothing, nothing, nothing to fear, except the fear itself,” alisema akimaanisha kuwa hakuna kitu chochote cha kuhofia zaidi ya hofu yenyewe.

“Wapuuzi wanakuja hapa, nimekuja nimesimama hapa halafu mtu anatoa bastola anasema rudi kwenye gari, nani amekupa mamlaka hayo?” alihoji Nape ambaye aliwahi kuwa katibu wa itikadi na uenezi wa CCM.

Nape alisema askari wanalipwa kutokana na kodi za wavuja jasho hivyo hawastahili kutisha watu.

“Do you know how I fought for this country (unajua nimepigania nchi hii kiasi gani)? Unajua nimekwenda miezi 28 nalala porini, angalia mkono wangu huu (akionyesha mkono wenye jeraha). Nimepigana kuirudisha CCM madarakani,” alisema.

“Anakuja mpuuzi anatoa bastola hapa, mimi mtoto wa Kimakonde na sitosimama.”

Nape alisisitiza kauli yake kuwa hana kinyongo na uamuzi wa Rais kwa kuwa hakuwahi kumshawishi amchague na hivyo hawezi kuhoji uamuzi wake.

“Lakini wakati anaunda baraza, walikuwapo watu wengi sana. Alipoamua kunichukua mimi, kuna watu walikuwapo na walikubali!, mimi leo nakatalia nini? Sina sababu ya kukataa,” alisema.

“Nimejitahidi kutimiza wajibu wangu. Na jana (juzi), wakati naongea na vyombo vya habari, wakati natoa ripoti nilisema kuna gharama ya kulipa kwenye kusimamia haki za watu. Na mimi niko tayari kulipa gharama hiyo.

“Sioni sababu kwa nini vyombo vinapaniki, sioni sababu kwa nini watu wapaniki, ni Mtanzania, Nape ni mdogo kuliko nchi, Tanzania yetu ni kubwa kuliko Nape. Tusihangaike na Nape, tuhangaike na Tanzania inakokwenda. Hilo ndilo kubwa kuliko yote.

“Uzalendo wa Nape kwa nchi yangu hauwezi kutiliwa mashaka hata kidogo na vijana wahuni wanaokuja hapa wananyoosha bastola kwa Watanzania walio huru. Nimekuwa mzalendo kwa nchi, nimekuwa muungwana kwa nchi yangu na ninaapa kuendelea kuwa muungwana kwa nchi yangu. Hilo hakuna atayelibadilisha

“Lakini mimi nimekuwa mzalendo kwa CCM ambayo niliikuta iko kwenye shimo inakwenda, nikasimama kuiinua. Watanzania wanajua. Uzalendo huo hauna mashaka hata kidogo. Na kwa uzalendo huo ndiko nilikoambiwa nitasema ukweli daima fitina kwangu mwiko.”

Alisema uzalendo huo alifundishwa na baba yake, Moses Nnauye ambaye alikuwa kada wa CCM na waziri wa zamani, ambaye alimfundisha kusema kweli.

“Na nilichokisimamia juzi ni kusema ukweli. Kinachokutanisha watu si magwanda ya kijani, ni imani kwamba tuwe wakweli, tuachane na fitina,” alisema Nape.

“Na hicho ndicho ninachokisamamia. Siwezi kukana, nikikana nihame.”

Nape alitaka vijana kusimamia haki na hakuna cha kuogopa.

“Kama ninachokiamini kitaleta matatizo, sina shida na wala si mara ya kwanza. Mnakumbuka mimi nilishawahi kufukuzwa CCM. Ndiyo, na katika maisha ya kisiasa usipopita kwenye migogoro bado hujakomaa,” alisema.

“Ili mbegu iote, lazima ioze. Sasa mbegu niliyoipanda, kwa hakika itaota. Vijana wa Tanzania, hamna cha kuogopa. Simamieni mnachokiamini. Tanzania ni yetu, nchi hii ni yetu. Mwalimu alikuwepo akaondoka. Kawawa na wenzake kina mzee Nnauye wakaondoka, na sisi tutaondoka.

“Suala la kujiuliza; tunawaachia Watanzania nchi gani. Hilo ndilo kubwa sana.”

Lengo la kuzungumza

Nape alisema lengo la kukutana na waandishi lilikuwa ni kumshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini kwa mwaka mmoja aliotumikia akiwa waziri na kumpongeza kwa uteuzi wake.

Alimshukuru kwa kumteua kuwa waziri bila ya kuanzia unaibu na kwamba Rais ameona inatosha na kumkabidhi kijiti Dk Mwakyembe.

“Yeye ni mwanahabari, ni mwanasheria ninamini atasimamia haki,” alisema.

Alishukuru pia vyombo vya habari kwa kumpa ushirikiano, wananchi wa Mtama waliompa ubunge na kwamba anaamini ametumia akili na nguvu zake zote kutekeleza majukumu aliyokuwa nayo.

“Nimefurahi kufanya kazi na nyie kwa dhati ya moyo wangu. Ninawaombeni muungeni mkono Waziri Mwakyembe aliyepewa dhamana ya wizara hii. Fanyeni naye kazi,” alisema.

“Lakini endeleeni kumuunga mkono Rais Magufuli, ndiye Rais tuliyenaye. Ndiye Rais tuliyepewa na Mwenyezi Mungu, ndiyo Rais tuliyempigia debe sisi Watanzania.”

Baada ya kumaliza kuzungumza, gari la Nape lilizuiwa na gari la polisi hatua chache baada ya kuondoka.

Mhariri wa gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile alisogea kwenye gari hilo na kumshauri Nape ashuke kwenda kuzungumza nao.

Baada ya muda alifanya hivyo kisha akarudi kwenye gari lake na kuwaomba wananchi na waandishi wa habari waliokuwapo eneo hilo, warudi majumbani kwao kwa ahadi kuwa kama kutakuwa na jambo jingine atawataarifu.

Utata wa mkutano

Awali walinzi wa hoteli ya Protea waliwataka waandishi watawanyike kwa madai kuwa ni agizo la Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Susan Kaganda.

Lakini Nape alituma ujumbe katika akaunti yake ya Tweeter kuwa mkutano uko kama ulivyopangwa na ilipofika saa 8:12 mchana Nape aliwasili kabla ya kutokea kwa rabsha hiyo.