Kisima cha Sh269 milioni hakijawahi kutoa maji Mpanda

Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jaffo 

Muktasari:

Kisima hicho kilichojengwa kwa miaka miwili kati ya mwaka 2013 hadi 2015 ili kuhudumia wananchi 1,600 waliopo kwenye kijiji hicho hawajawahi kunufaika nacho.

Dodoma. Licha ya kuchimbwa na kugharimu Sh268.9 milioni, kisima kilichopo Kijiji cha Ngomalusambo wilayani Mpanda, hakijawahi kutoa maji.

Kisima hicho kilichojengwa kwa miaka miwili kati ya mwaka 2013 hadi 2015 ili kuhudumia wananchi 1,600 waliopo kwenye kijiji hicho hawajawahi kunufaika nacho.

Akieleza sababu za changamoto za visima vingi kutotoa maji licha ya kukamilika kwake kama ilivyokusudiwa, leo (Jumatano) Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jaffo amesema hujuma za wananchi dhidi ya miundombinu hiyo zinachangia kukithiri kwa changamoto hiyo.

Akijibu swali la Mbunge wa Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso juu ya kutonufaika kwa wananchi wake na mradi huo, naibu waziri huyo amesema hatua stahiki zimechukuliwa.

"Mradi umeshindwa kutoa huduma kutokana na kuibwa kwa betri ya pampu. Kukabiliana na changamoto hiyo, halmashauri imenunua betri mpya na kuifunga," amesema Jaffo.

Licha ya hilo, serikali imesema Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda ina mpango wa kuchimba kisima kingine mwaka ujao wa fedha baada ya kisima kilichopo kupoteza uwezo wake.