Kisiwa cha Bongoyo hatarini kutoweka

Sehemu ya kisiwa cha Bongoyo kilichopo Bahari ya Hindi kikiwa kimemegwa na maji

Muktasari:

Kaimu Mhifadhi Mfawidhi wa maeneo tengefu Mkoa wa Dar es Salaam, Jairos Mahenge amesema kuna haja ya kufanya  tafiti ili kupata suluhu kuhusu  nanma ya kukabiliana na mabadiliko hayo.

Dar es Salaam. Mabadiliko ya hali ya hewa yanaendelea kukiathiri Kisiwa cha Bongoyo kilichopo jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mhifadhi Mfawidhi wa maeneo tengefu Mkoa wa Dar es Salaam, Jairos Mahenge amesema kuna haja ya kufanya  tafiti ili kupata suluhu kuhusu  nanma ya kukabiliana na mabadiliko hayo.

“Kina cha maji ya Bahari ya Hindi kinazidi kupanda na pepo hazitabiriki…kisiwa kinaonekana kumezwa, hali hii inahatarisha hata utalii wa hapa,” amesema.

Tofauti na kisiwa kilichopo jirani cha Mbudya, Bongoyo hutembelewa idadi kubwa ya wageni kutoka nje ya nchi lakini wahifadhi wanahofia huenda mandhari inayowavutia watalii ikamezwa na bahari.

Kiongozi wa Wahifadhi wa Kujitolea Bongoyo, John Mbuwa amesema ardhi ya kisiwa hicho inaendelea kumomonyoka, jambo lililosababisha kuhamisha banda lao la kuhudumia watalii baada ardhi kumomonyolewa na maji.

Mfaume Majaliwa ambaye ni Mhifadhi wa Kujitolea katika Kisiwa cha Mbudya amesema uchafu wa mazingira Dar es Salaam unahatarisha mandhari ya visiwa hivyo hasa wakati wa masika.

“Uchafu wote unaletwa na maji ya mvua huingia baharini. Hali hii sio nzuri kabisa na watalii hawapendelei. Programu ya usafi ni muhimu iwapo tunataka watalii waendelee kuja kwenye visiwa hivi,” amesema Majaliwa.

Hata hivyo, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imeanza mkakati wa kuvitangaza visiwa hivyo kwa ajili ya kuwavutia watalii zaidi tofauti na sasa Mlima Kilimanjaro, Visiwa vya Zanzibar na hifadhi za wanyama zilizopo kaskazini mwa nchi hutangazwa zaidi.

Kwa kujibu wa Ofisa Masoko wa TTB, Francis Malugu, mkakati uliopo ni kutangaza utalii wa kitamaduni na kuhamasisha Watanzania kufanya utalii wa ndani.