Monday, December 10, 2012

Mkapa ang’ata wasiotekeleza ahadi majimboniRais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa

Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa 

By Burhani Yakub na Raisa Said Lushoto

RAIS Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa amewakoromea baadhi ya viongozi waliotoa ahadi mbalimbali kwa wananchi na kushindwa kuzitekeleza na kusema wamewaahidi upuuzi.
Mkapa aliyeingia madarakani 1995 hadi 2005, alisema: “Viongozi wa kisiasa  waliotoa ahadi za kuwaletea maendeleo wananchi wakati wa kampeni za kuomba kupigiwa kura wakashindwa kuzitekeleza, walikuwa wakifanya upuuzi kwani waliwaahidi wananchi yasiyowezekana.”

Kiongozi huyo aliyasema hayo wakati wa mahafali ya tatu ya Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU) yaliyofanyika katika ukumbi mpya wa chuo hicho wilayani hapa.
Hatua ya Mkapa imekuja ikiwa ni mara kadhaa viongozi mbalimbali wakiwamo Wabunge wamelalamikiwa kwa kushindwa kutekeleza ahadi mbalimbali walizotoa kwa wapiga kura wao.

Wabunge wengi katika majimbo yao wamekuwa wakilalamikiwa kwa kushindwa kutatua kero za maji safi na salama hususan maeneo ya vijijini na wananchi wanahangaika kila kukicha bila msaada wa wabunge wao. Mbali na maji wananchi wamekuwa wakilalamikia masuala ya afya ya msingi kuwa wengi wa wananchi vijijini wanatembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo katika zahanati na vituo vya afya ambavyo navyo vinakabiliwa na uhaba wa dawa.

Kero nyingine ni kukosekana kwa utatuzi wa uhaba wa walimu, madawati, nyumba za walimu, vitabu vya ziada na kiada.

Kwa upande wa kilimo, changamoto kubwa zinazowakabili wananchi ni gharama za pembejeo huku idadi ya vocha za ruzuku, ukosefu wa masoko ya uhakika kwa mazao mbalimbali ya biashara ambayo wabunge wengi wamekuwa wakitumia hayo kujinadi kumaliza matatizo.

Akiwa amefuatana na mkewe Mama Anna, Mkapa alisema imejengeka tabia siku hizi baadhi ya watu kutafuta uongozi wa kisiasa na jamii kwa madai kwamba watawaletea wananchi maendeleo jambo ambalo si rahisi kulitekeleza kwa vyovyote.“Ahadi za namna hii ni upuuzi mtupu, tuliaswa na uongozi wa rika ya Baba wa Taifa, Mwalimu  Julius Nyerere kwamba kupatikana maendeleo kuna masharti yake lazima kuwe na Watu, Ardhi, Siasa safi na Uongozi bora na hapa mimi naongezea mtaji,” alisema Mkapa katika mahafali hayo na kushangiliwa na wanachuo.

Rais huyo mstaafu alisema mkusanyiko na ushirikiano wa masharti hayo ndiyo unaleta maendeleo na si kwa Mbunge kuwaletea maendeleo wananchi, hiyo haiwezekani na haipo.

Alisema asilimia 40 ya kaya za Watanzania Bara hazina vyoo vya kisasa na huko ni kukosekana kwa maendeleo na alihoji kama  kuna mgombea ubunge aliyeijenga katika  kila kaya kwenye jimbo lake choo cha kisasa.

“Kuna mgombea gani wa ubunge amejenga au kuziletea kaya zote za jimbo lake choo cha kisasa?,” alihoji Mkapa ambaye alisema kinachowezekana katika kuleta maendeleo ni kwa nguvu za wananchi wanaojitolea kukusanya nguvu zao kwa ushirika na kufanya kazi.

Alisema wingi wa wananchi ndiyo utakaoleta maendeleo kwa kurahisisha kazi na siyo majigambo ya wanaovizia uongozi hata kama wangelikuwa wamesoma kiasi gani.

Katika mahafali hayo, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (TUMA), Profesa Esther Mwaikambo aliwatunuku wahitimu wa Shahada, Stashahada na Astashahada katika nyanja za sheria, sayansi na elimu kwa wahitimu 400.

Akizungumza katika mahafali hayo, aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Sebastian Kolwa  (SEKUco) ambacho kimepanda hadhi na kuwa chuo kikuu kamili, Mchungaji Dk Anneth Munga alisema chuo hicho kipo katika mikakati mbalimbali ya kuboreshwa ili kitoe elimu bora nchini.

-->