Monday, March 4, 2013

Wahandisi washirikishwe kutatua matatizo

By Fredy Azzah

Matatizo yanayoikabili sekta ya uandisi nchini yatapatiwa ufumbuzi endapo wahandisi watashirikishwa na kupewa kipaumbele.

Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania,  Dk Malima Bundara alisema jambo la msingi ni kujadili umuhimu wa wahandisi katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hiyo.

Baadhi ya matatizo ni sababu zinazozuia maendeleo ya kiuchumi ikiwamo  ajira, elimu, ukiukwaji wa taratibu zinazoendana na fani ya uhandisi na matumizi mabaya ya rasilimali.

“Tusijidanganye kuwa wahandisi wa kigeni watatoa ufumbuzi wa muda mrefu wa matatizo tuliyonayo kama nchi. Hawa wamekuja kutafuta fedha na kurudi nazo kwao,” alisema Dk Bundara.

Dk Bundara aliitaka serikali iwatumie wahandisi wazalendo kutafuta ufumbuzi mtatizo mbalimbali yanayorudisha nyuma maendeleo ya  nchi.

“Kama serikali na taasisi zake itawatumia vizuri wahandisi wazalendo, mapinduzi ya haraka katika uchumi wa nchi yatapatikana,” alisema Bundara.

Kwa upande wake, Mhandisi Ladislaus Salema ambaye ni  Rais wa zamani wa taasisi hiyo, alishangaa ni kwa nini nchi iliyobarikiwa kuwa na rasilimali na maliasili za kutosha kama Tanzania, bado inapata shida katika kutengeneza ajira kwa wananchi wake,  na bado imeorodheshwa katika nchi zinazoendelea.

-->