Tuesday, March 12, 2013

Waandishi, dola kukutana kujadili usalama

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya habari nchini (Moat), Reginald Mengi akitoa tamko la maazimio Chama hicho kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kujeruhiwa kwa Mhariri Mtendaji wa New Habari Corporation Absalom Kibanda,ambaye anatibiwa nchini Afrika Kusini.Picha na Silvan Kiwale 

By Bakari Kiango,Mwananchi

Dar. Wadau wa habari wameunda kamati ya watu 16 itakayokutana na wakuu wa vyombo vya usalama nchini, kuzungumzia kwa undani suala la usalama wa makundi yanayoshambuliwa, kuumizwa na kuuawa wakiwamo waandishi wa habari.


Kamati hiyo inajumuisha Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi (MCL), Tido Mhando, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (Moat), Reginald Mengi na Katibu wake, Henry Muhanika.


Wajumbe wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa New Habari (2006) Limited, Hussein Bashe, Meneja Mkuu wa Business Times, Aga Mbuguni, Meneja Mkuu Global Publishers, Abdallah Mrisho na Mhariri Mtendaji wa Free Media, Ansbert Ngurumo.


Wengine ni Mhariri Mkuu Nipashe, Jesse Kwayu, Mkurugenzi Uhuru Publishers, Mikidadi Mahamoud, Godfrida Jola kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Japhet Sanga kutoka Tanzania Media Fund (TMF), Nevile Meena kutoka Jukwaa la Wahariri (TEF), Pili Mtambalike Baraza la Habari Tanzania (MCT), Tumani Mwailenge MisaTan, Deodatus Balile gazeti la Jamhuri na Samson Kamalano gazeti la Changamoto.


Akisoma maazimio baada ya mkutano wa wadau wa habari uliokuwa na lengo la kujadili hali ya kuzorota kwa mazingira ya usalama ya waandishi wa habari na wanaharakati wengine, Meneja wa Business Times, Aga Mbuguni alisema wanaamini kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Tef, Absalom Kibanda kumetokana na msimamo imara wa kalamu yake.


“Shambulio lililofanywa dhidi ya Kibanda halikutokana na kitu kingine chochote zaidi ya kazi yake ya uandishi wa habari. Wadau wamelichukua suala hili kuwa, ni shambulizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari nchini na kuwajengea hofu wahariri, waandishi na wanaharakati wote ili wasitekeleze wajibu wao kwa umma,” alisema Mbuguni.


Naye Mwailenge kutoka MisaTan, alisema tukio hilo ni mfululizo wa mashambulizi ya namna hiyo na kwamba, mazingira hayo wamejiona na kutambua kuwa hakuna aliye salama.
“Ilianza kwa waandishi wa habari wa gazeti la Mwanahalisi, Saed Kubenea na Ndimara Tegambwage, kutekwa kwa Dk Steven Ulimboka, kuuawa kwa mwandishi wa kituo cha Channel Ten Daudi Mwangosi na mashambulizi ya Kibanda,” alisema Mwailenge.


Naye Kwayu alisema wamesikitishwa na hatua ya baadhi ya maofisa na watumishi wa vyombo vya usalama, kutumiwa kutekeleza vitendo vya uhalifu ambavyo vinatishia usalama wa waandishi wa habari na wananchi.


“Usumbufu alioupata mwandishi Shinani Kabendera wa mkoani Kagera na familia yake, walihojiwa na waliojiita watumishi wa idara ya uhamiaji, ulifanywa kwa shinikizo la watu,” alisema Kwayu.


Kwa upande wake, Bashe aliitaka Serikali iunde tume huru ya wapelelezi kuchunguza undani wa masuala hayo, kwa sababu kasi ya uchunguzi wa vyombo vya usalama nchini hairidhishi na baadhi ya watendaji ndani ya vyombo hivyo wanahusishwa.

-->