Wednesday, March 13, 2013

Wanaharakati, wasomi wazidi kuisakama Serikali

 

By Kelvin Matandiko,Mwananchi

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema Serikali ya awamu hii itasalia kumbukumbu ya matukio ya ukiukwaji wa demokrasia.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa LHRC, Dk Helen-Kijo Bisimba alisema taifa limebadilika, amani imeanza kutoweka miongoni mwa Watanzania huku serikali ikiwa na vyombo vyote vinavyohusika na masuala ya ulinzi na usalama wa raia.

“Usalama umepungua na serikali hatuoni juhudi za kushughulikia kikamilifu, siamini kama imeelemewa na uovu huu, kama ni kuelemewa ijipange upya itafute mbinu mbadala kurejesha imani kwa Watanzania,” alisema Dk Bisimba.

Kauli hiyo imekuja zikiwa ni siku chache la kujitokeza kwa tukio la utekaji na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), Absalom Kibanda.

Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Saikolojia ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa), Dk Kitila Mkumbo alisema taifa kwa sasa linaelekea kufuata misingi ya utawala wa kiimla.

Profesa Gaudence Mpangala alisema Serikali imekosa uvumilivu wa kidemokrasia, kutokana na baadhi ya matukio yanayoashiria kuhusika moja kwa moja.  “Ukiangalia utekaji wa Ulimboka mazingira yalionyesha wazi kabisa  hakuna ukweli walioutoa, kinachotakiwa kama hawakuhusika basi watuonyeshe ukweli wa tukio,” alisema.

-->