Wednesday, March 20, 2013

Lwakatare aachiwa, kisha akamatwa tena

Mkuu wa Usalama wa Chama cha Demokrasia na

Mkuu wa Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),Wilfred Lwakatare 

By Waandishi Wetu, Mwananchi

Mkuu wa Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura wamefutiwa mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yanawakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuachiwa huru, lakini walipotoka nje ya chumba cha mahakama “wakakamatwa tena”.


Habari kutoka mahakamani Kisutu zinasema kuachiwa kisha kukamatwa tena kwa watuhumiwa hao kunatokana na makosa ya kisheria yaliyofanywa wakati waliposomewa mashtaka kwa mara ya kwanza.


Makosa hayo ni pale washtakiwa walipoulizwa iwapo wanakubali au wanakana makosa yao, hali mahakama ya Kisutu ikiwa haina uwezo wa kusikiliza kesi za ugaidi.


Washtakiwa hao waliachiwa huru jana saa 3.00 asubuhi na Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru baada ya Wakili wa Serikali, Prudence Rweyongeza kuwasilisha hati kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akiiomba mahakama kuwaachia chini ya kifungu cha 91 (1).


Kifungu hicho kinampa mamlaka Mkurugenzi huyo wa Mashtaka kufuta mashtaka pale anapoona hana sababu ya kuendeleza mashtaka ya mtuhumiwa bila hata ya kutoa sababu zilizosababisha kufanya hivyo.

Hakimu Mchauru alikubaliana na hati hiyo na kuwafutia mashtaka washtakiwa hao waliokuwa wanakabiliwa na kesi namba 37 ya mwaka 2013, iliyokuwa na mashtaka manne yanayohusu vitendo vya ugaidi.

Hata hivyo, baada ya mshtakiwa huyo kuachiwa huru na Hakimu Mchauru, alipotoka nje ya chumba cha mahakama, askari ambao walikuwa wamevaa sare na nguo za kiraia walimkamata Lwakatare ambaye aligoma kukamatwa akidai hadi awepo wakili wake.

Baadaye alifika wakili wake, Peter Kibatala hivyo alikubali kuwekwa chini ya ulinzi. Hivyo askari walimchukua na alipofika karibu na mahakama ya wazi, alifungwa pingu na baadaye kwenda kuhifadhiwa ndani ya gari la polisi akiwa chini ya ulinzi mkali.

Ilipofika saa 4:10 asubuhi, Lwakatare na mwenzake, Ludovick walipandishwa tena kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana na kusomewa kesi mpya PI namba 96 yenye mashtaka manne yanayofanana na yale ya awali ya ugaidi.

Akisoma hati hiyo mpya ya mashtaka, Wakili Rweyongeza alidai kuwa washtakiwa hao walifanya kosa hilo la jinai kinyume na kifungu cha 384 cha sheria ya kanuni ya adhabu, sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho 2002.

Rweyongeza alidai kuwa Desemba 28, mwaka jana katika eneo la King’ong’o, Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kumdhuru kwa sumu Dennis Msacky ambaye ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, kinyume na kifungu cha 227 cha sheria ya kanuni ya adhabu.

Wakili huyo wa Serikali katika shtaka la pili alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kufanya kosa la jinai kinyume na kifungu cha sheria cha 24 (2) cha sheria dhidi ya ugaidi sura ya 21 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Alidai kuwa washtakiwa hao, Desemba 28,2012 walishirikiana kupanga njama za kumteka nyara Msacky kinyume na kifungu cha 21 cha sheria inayopinga ugaidi.

Katika shtaka la tatu, wanadaiwa kufanya mkutano wa vitendo vya kigaidi kinyume na kifungu cha 5 (a) cha sheria namba 21 inayopinga ugaidi iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Aliendelea kudai kuwa siku ya tukio, washtakiwa hao walipanga na kushiriki katika mkutano wa kupanga kitendo cha ugaidi cha utekaji nyara dhidi ya Msacky.

Kwa mujibu wa shtaka la nne, Lwakatare anadaiwa kuhamasisha vitendo vya ugaidi.
Aliongeza kudai kuwa siku hiyo ya tukio, Lwakatare akiwa mwenye nyumba, akijua, aliruhusu mkutano kati yake na Ludovick ufanyike katika nyumba yake kwa lengo la kuhamasisha vitendo vya kigaidi dhidi ya Msacky.

Kabla ya kufutwa kwa kesi hiyo, Hakimu Mchauru alitakiwa kutoa uamuzi kama washtakiwa hao watapata dhamana ama la, kutokana na hoja zilizokuwa zimewasilishwa na mawakili wa pande zote mbili.

Hata hivyo, suala hilo halikujadiliwa baada ya Hakimu Katemana kusema kwamba hakuwa na muda wa kulisikiliza kwani alikuwa anawahi kesi nyingine.Kesi hiyo sasa imeahirishwa hadi April 3, mwaka huu na mawakili wa pande zote mbili watapata fursa ya kujadili suala hilo.

Lwakatare anatetewa na mawakili watano, Peter Kibatala, Mabere Marando, Abdallah Safari, Nyaronyo Kicheere na Tundu Lissu.

-->