Friday, March 29, 2013

Rais Kikwete, Maalim Seif waongoza mazishi ya mbunge

Wabunge,  ndugu na jamaa wa marehemu Salim

Wabunge,  ndugu na jamaa wa marehemu Salim Hemed Khamis aliyekuwa Mbunge wa Chambani (CUF) wakiutoa mwili wake baada ya kuagwa rasmi  katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, jana. Picha na Emmanuel Herman. 

By Masanja Mabula, Mwananchi

Pemba. Mbunge wa Chambani, Salim Hemed Khamis amezikwa kijijini kwake Mizingani.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Sief Sharif Hamad aliongoza mamia ya wananchi kwenye mazishi hayo.

Awali, Rais Jakaya Kikwete aliongoza mamia ya wakazi wa Dar es Salaam kuaga mwili wa Mbunge wa Chambani,  Salim Hemed Khamis (CUF) kwenye viwanja vya Karimjee, aliyefariki dunia juzi Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Akitoa salamu za Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema Bunge limepoteza mtu shupavu ambaye alikuwa mchangiaji mzuri  kwa kutoa hoja zenye lengo la kujenga.

Lukuvi aliwataka wananchi wa  Chambani kuwa wastahimilivu wakati huu wa msiba, baada ya kuondokewa na kiongozi wao mpendwa.

Alisema licha ya kuwa mbunge  wa upinzani, lakini hoja zake zililenga kukosoa Serikali na kurekebisha na kwamba, pale alipobaini upungufu na daima hakusita.

Akizungumza kwa niaba ya  familia, Mbunge wa Mtambilem Masoud Salim alisema Serikali zote mbili na uongozi wa Bunge wamefanya kazi mzuri kuanzia hospitali hadi maziko yake.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa  Ibrahim Lipumba alisema chama chake kimepoteza kiongozi na mwanachama mzuri na kwamba, itakuwa vigumu kuziba pengo hilo.

Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Edward Lowassa na viongozi mbalimbali.

Awali, viongozi waliohudhuria kutoa heshima za mwisho mjini Dar es Salaam, ni Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilibrod Slaa na wabunge mbalimbali.

Akisoma historia fupi ya marehemu Khamis, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema kulingana na taarifa za madaktari alikuwa anasumbuliwa na shinikizo la damu.

-->