Saturday, March 15, 2014

Kinana: Wasaliti CCM wako kumi

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, akisisitiza jambo kwenye moja ya mikutano yake aliyoifanya hivi karibuni. Picha na Maktaba 

By Kizitto Noya, Mwananchi

Dodoma. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amesema hana mpango wa kuwahoji Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotokana na chama hicho kwa sababu ya misimamo yao inayokinzana na miongozo ya chama, kwa kuwa anawafahamu wote kwa majina na idadi yao haizidi kumi.

Kauli hiyo ya Kinana inafuatia taarifa zilizoripotiwa na gazeti hili hivi karibuni kuwa, CCM kimeanza kuwahoji baadhi ya wabunge wake, ambao ni Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu ya kupingana na maelekezo ya chama hicho kuhusu Muundo wa Serikali mbili.

 “Sisi (CCM) hatuhoji mtu kwa sababu ya kuwa na msimamo tofauti, kwani hawa wenye msimamo tofauti na chama hawazidi kumi ama siyo zaidi ya 15,” alisema Kinana na kuongeza;

“Hawa watu mimi nawajua kwa majina, mmoja (jina tunalo) ni hatari zaidi kwa sababu anaweza kuwakusanya wengine na kuwashawishi wafuate msimamo wake, lakini waliobaki wote, hawatishi kwa kuwa wanabaki na misimamo yao wenyewe.”

Kwa mujibu wa habari hiyo, wajumbe waliohojiwa ni wale wanaotokana na Ubunge wa Jamhuri ya Muungano na ambao wanataka Muundo wa Serikali tatu. “Ni kweli hata mimi niliitwa na akaniambia (mwakilishi wa chama) ametumwa aniletee ujumbe kuwa niko kwenye orodha ya watu 90 na nikiendelea na msimamo wangu nitachukuliwa hatua,” alieleza mmoja wa wajumbe waliodai kuwa wamehojiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.

Maelezo ya Kinana

Kinana aliliambia gazeti hili kuwa, kulingana na muundo wa chama hicho tawala, viongozi wanaoweza kuwahoji watu ni yeye Katibu Mkuu, Makamu Mwenyekiti, Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM, Waziri Mkuu na Mwenyekiti wa chama Taifa. “Tena tunafanya hivyo kwenye vikao maalumu na kwa sababu ambazo haziwezi kuwa siri.”

Kinana alieleza kuwa taarifa kwamba CCM imewahoji watu 90 kutokana na kuwa na misimamo tofauti na chama hicho kuhusu Serikali mbili na kura ya wazi, siyo za kweli na anaamini imesambazwa na watu kwa malengo yao binafsi. Kinana anafafanua kuwa CCM kama chama kikubwa nchini chenye wafuasi karibu nchi nzima, hakiwezi kudhibiti mitizamo ya watu na kimsingi tofauti za mitazamo ndiyo msingi wa demokrasia.

Novemba 20 mwaka 2012 akizungumza katika kipindi cha Jenerali on Monday kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Kinana alitoa onyo kwa makada wasaliti kuwa atasimamia utekelezaji wa uamuzi wa Halmashuari Kuu ya CCM (Nec) ya kuwabaini na kuwaondoa viongozi wanaokwenda kinyume na matakwa ya chama na kukipaka matope.

Kura ya wazi na Serikali mbili

Katika hatua nyingine, Kinana alizungumzia msimamo wa chama hicho wa kura ya siri na muundo wa Serikali mbili, akieleza kuwa siyo jambo la ajabu, kwani katika mchakato wa kutunga katiba, kila kundi lina maoni na mtazamo wake na kuutetea kwenye mijadala.

“Wanaosema kuna vyama havina msimamo pale bungeni ni waongo. Siyo vyama tu, kila kikundi kina msimamo unaotokana na uchambuzi wao wa hali ya siasa nchini na wanachofikiri kina masilahi kwa nchi na watu wanaofuata mtazamo wao. Hawawezi kuniambia kama Lipumba (Profesa Ibrahim) na Mbowe (Freeman), hawana wanachosimamia kwenye mjadala huo wa Bunge Maalumu,” alisema na kusisitiza:

“Watanzania wasitarajie miujiza, lazima mivutano ya aina hiyo iwepo, kwani kila kundi linajitahidi kupenyeza mawazo yake na wanaoitetea misimamo hiyo ni watu. Kikubwa hapa sasa ni uvumilivu, watu wavumiliane na wazungumze kwa hoja na mwisho wa yote wafikie mwafaka.”

Alipoulizwa kama ni kweli CCM imekuwa ikiwashinikiza wajumbe wake kusimamia matakwa ya chama hicho, alijibu “Siyo CCM tu, CUF wanakutana na Chadema wanakutana, tena kila siku. Hili ni jambo la kawaida.”

Anasema tatizo siyo chama kuwa na msimamo, bali chama kutokukubali kubadili misimamo yake hata kama haikuwa sawa. Unaweza kuwa na msimamo wako, lakini ukaja mbele ya wenzako, ukagundua kuwa hauko sahihi, ikifikia hapo unapaswa kulegeza kamba ili uingize mawazo ya wenzako pia kwenye hoja zako, alisema.

Wito kwa Wajumbe wa Bunge la Katiba

Kinana ametoa wito kwa Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba akiwataka watambue kuwa Tanzania siyo nchi ya kwanza kutengeneza katiba.

Alisema zipo nchi nyingi duniani, ikiwamo India, Indonesia, Columbia, Kenya na Pakistan ambazo zilitumia muda mrefu zaidi kutunga katiba zao.

“Sisi kutumia majuma matatu kutengeneza kanuni za kuongoza Bunge Maalumu la Katiba, ni hatua nzuri tunayopaswa kujivunia,” alisema.

Kinana aliendelea kueleza kuwa pamoja na tofauti zinazojitokeza katika mijadala ya Bunge hilo Maalumu, makundi yanayounda Bunge hilo yanapaswa kutambua utaifa na uzalendo na ikilazimika waache tofauti zao ili wawe na mwelekeo wa pamoja katika kufikia mwafaka unaokusudiwa.

“Kwa hali hiyo pamoja na tofauti zetu, tusiondoke kwenye lengo. Mimi naamini katiba tunayoitaka itapatikana ila safari ya kuipata ni ndefu na ngumu.”

-->