Monday, March 30, 2015

Viongozi wa dini waiweka Serikali pabaya kuhusu Katiba Mpya

 

By Florance Majani

Dar es Salaam. Viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu wameendelea kuiweka Serikali katika wakati mgumu baada ya kusema hawataiunga mkono Katiba Inayopendekezwa ikiwa matakwa yao hayatazingatiwa.

Akizungumza jana ikiwa ni siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema viongozi wa dini walitoa matamko ya hasira na yasiyokuwa na tija walipowataka wananchi kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, (TEC),Askofu Severin Niwemugizi alisema kulazimisha Katiba ipite kama ilivyo ni udhaifu mkubwa kwa sababu ina upungufu mkubwa ambao hautaweza kurekebishwa baadaye.

“Naikataa kwa asilimia 100. Kwa kifupi, Rais akubali kutokukubaliana na sisi.”

Wakati askofu huyo akisema hayo, Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Simba amesema iwapo Serikali haitaitambua Mahakama ya Kadhi na makadhi, Waislamu wataususia mchakato wa upigaji wa kura ya maoni kupitisha Katiba Inayopendekezwa.

Askofu Niwemugizi

Akizungumzia kauli hiyo ya Rais Kikwete, Askofu Niwemugizi alisema msimamo wa Jukwaa la Wakristo wa kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa haukuwa wa hasira, bali uliangalia kwa mapana masilahi ya Taifa katika miaka 200 ijayo.

Alisema ni udhaifu mkubwa kulazimisha kuipitisha Katiba ikiwa na upungufu na kusisitiza kuwa inatakiwa kutengenezwa kwa ustadi kwa sababu inagusa maisha ya Watanzania.

“Anaposema tamko letu lilikuwa la hasira na kuwa tuwaache wananchi waamue wenyewe anakosea kwa sababu Serikali yenyewe tangu ilipoizindua ilikuwa inawahamasisha wananchi waipigie kura ya ndiyo.

“Rais anaposema tusiwaamulie wananchi anakosea kwani hata sisi ni wananchi, lakini pia kutokana na nafasi zetu tunawawakilisha wananchi ambao hawana elimu, tuna wajibu wa kuwafundisha wasioelewa, wasiojua kusoma wala kuandika.”

Aliilaumu Serikali kwa kuipitisha Katiba hiyo mapema kabla haijaeleweka kwa wananchi.

Mufti anena

Mbali ya kutishia kususia mchakato wa kupitisha Katiba Inayopendekezwa, Sheikh Mkuu alisema Serikali haitatenda haki iwapo italiacha suala la Mahakama ya Kadhi mikononi mwa taasisi za kidini na kuitaka iitambue.

“Mbona CCM ililiweka hilo katika ilani ya uchaguzi mwaka 2010, halafu leo waseme kuwa wanatuachia wenyewe suala la Mahakama ya Kadhi? Hii si haki hata kidogo,” alisema Mufti Simba.

“Kama msimamo ndiyo huo basi sisi tutaendelea kuidai Mahakama ya Kadhi kama ambavyo tumekuwa tukisema siku zote na hatutaipigia kura hiyo katiba,” alisema alisema.

Kadhalika, alitaka Serikali kuacha kuliendesha suala la Mahakama ya Kadhi, ki- Bakwata Bakwata (Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania), bali ihusishe pia taasisi na jumuiya zote za Kiislamu ambazo zinawaunganisha Waislamu wote nchini.

Katika mkutano huo wa juzi, ulioandaliwa na Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam na kuwashirikisha wajumbe mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo, Rais Kikwete alisema; “mwelekeo wa mambo hauhitaji uwe bingwa kujua hali hairidhishi, iwapo hatua hazitachukuliwa kutakuwa na uvunjifu wa amani wa kidini ambao moto wake ni mkali.”

-->