Amedumu Msondo Ngoma miaka 45

Saturday November 17 2018

Mpiga solo mahiri wa Msondo Ngoma Music Band,

Mpiga solo mahiri wa Msondo Ngoma Music Band, Said Mussa Mabela 

By Mohammed Kuyunga, Mwananchi

Hii inaweza kuwa historia nchini kama si duniani. Mpiga solo mahiri wa Msondo Ngoma Music Band, Said Mussa Mabela amedumu na bendi hiyo kwa takribani miaka 45 sasa.

Mabela hajawahi kuihama bendi hiyo tangu alipojiunga nayo mwaka 1973.

Mwanamuziki huyo ambaye ni mahiri katika upigaji wa gitaa la solo, asili yake ni mkoani Kigoma alifikia hatua ya kuiongoza bendi hiyo na kukumbana na misukosuko mingi.

Mabela alifundishwa kupiga gitaa la solo na babu yake, Pili Shaban aliyekuwa mwanamuziki wa Bendi ya Lake Jazz ya Kigoma. “Wakati huo nilikuwa nasoma Shule ya Msingi ya Kipampa, nilikuwa naenda kwake maeneo ya Gungu ananielekeza jinsi ya kupiga gitaa,” anakumbuka Mabela.

Mara baada ya kumaliza shule ya msingi, Mabela hakuendelea na masomo akili yake ilishaelekea kwenye muziki na kuanza kutafuta bendi ya kupigia.

“Nikiwa katika harakati hizo, nilitoka Kigoma na kwenda Tabora, nilifika pale na kukaa kigodo katika Bendi ya Tabora Jazz kisha nikaelekea Musoma Jazz,” anasema.

Hata hivyo, mwanamuziki huyo ambaye ni mtoto wa sita katika familia ya Mzee Mussa Mabela hakudumu Musoma Jazz.

MNENGE AMLETA NUTA JAZZ

“Nilikuwa nimerudi nyumbani Kigoma kwa likizo ndipo nilipokutana na Mpiga Saxphoni wa Nuta Jazz, Mnenge Ramadhani.

“Nilimwambia anifanyie mipango nijiunge na Nuta naye akanitaka niende Dar es Salaam.”

Baada ya kuambiwa hivyo, Mabela hakutaka kulaza damu akafanya mipango na kutua Dar es Salaam.

APEWA UJUMBE NA MZEE MWILIMA

Mabela anasema alitafuta nauli ya kwenda Dar es Salaam kwa nguvu zote na alipofanikisha alipokelewa na Mnenge aliyemuunganisha kwa aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Elimu ya Nuta, Aboubakary Mwilima.

“Mzee Mwilima aliniandikia ujumbe katika karatasi na kunitaka niupeleke kwa kiongozi wa bendi pale kwenye Ukumbi wa Amana ili nifanyiwe usaili.”

Mabela anasema alipopewa nafasi ya kufanya usahili huo hakutaka kufanya makosa, alifanya vizuri na wahusika waliridhika na uwezo wake.

ALIOWAKUTA WOTE HAWAPO

Kitu ambacho kinamsikitisha, Mabela ambaye maarufu anajulikana kwa jina la Dokta ni kuwa wanamuziki wote aliowakuta wakati anajiunga na Nuta Jazz wote wameshafariki dunia. “Labda Mohammed Omary ‘Kajamba’ ndiye ambaye sina uhakika kama bado yuko hai au amefariki dunia lakini wengine wote hatuko nao,” anasema.

Wanamuziki aliowakuta Nuta Jazz na vyombo wanavyopiga kwenye mabano ni Abel Bartazal (solo), Kiiza Hussein (second solo), Ahmed Omary (bass) na Hamis Sama.

Pia, Mabela anakumbuka Nuta wakati huo ilikuwa na waimbaji wawili tu, Muhidin Maalim Gurumo na Juma Akida na wakati mwingine walisaidiwa na Joseph Lusungu ambaye alikuwa akipiga trumpert.

Itaendelea wiki ijayo...

Wanamuziki wengine ni Mnenge na Juma Town (sax), Kajamba (tumba) na Mabruki Khalfan (drums).

APIGWA ZENGWE, AHAMIA KWENYE TRUMPERT

Aidha, Mabela anakumbuka wakati akiingia katika bendi hiyo alikutana na misikosuko kutoka kwa kiongozi wa bendi na mpiga solo, Bartazali.

“Hakutaka nipige gitaa la solo, alitaka kupiga peke yake nyimbo zote, nikamwachia. Nikahamia kwenye trumpert,” anasema.

Mabela anazikumbuka baadhi ya nyimbo ambozo alishiriki kupiga trumpert kuwa ni Hebu Sikia, Nisingekumbia.

Aidha mwanamuziki huyo anasema ilifika hatua Bartazali alichoka kupiga peke yake na kumuomba amsaidie ndipo aliporudi kwenye gitaa hilo la solo.

ALITAKIWA DAR INTERNATIONAL

Mabela anafichua kulikuwa na mpango wa baadhi ya wanamuziki wa Nuta Jazz mwaka 1977 kwenda kuanzisha Bendi ya Dar International.

“Katika mpango ule nilikuwapo mimi, Gurumo na Abel ( Bartzali) lakini haukufanikiwa aliondoka Abel peke yake,” anakumbuka.

Mabela anasema Bartazali alikuwa ndiye anayewasiliana na mmiliki wa Bendi ya Dar International Zacharia na alikuwa akipewa pesa za kuwafikishia yeye na Gurumo lakini hawakufanikiwa kuzipata.

“Pesa zote alikuwa akichukua peke yake, ndipo alipolazimishwa kuhama na kwa kuwa siye hakutupa pesa tukabaki Nuta,” anakumbuka.

Alipoondoka Bartzali ndipo, Mabela aliuomba uongozi wa bendi umtafutie msaidizi na akapatikana Kassim Mponda.

AKABIDHIWA UONGOZI

Mabela ni mwanamuziki ambaye amekuwa kiongozi katika bendi ya Msondo Ngoma kwa muda mrefu zaidi.

Alipewa cheo hicho mwaka 1977 baada ya kuondoka kwa Bartazali na alidumu nacho hadi pale aliporudi tena katika bendi hiyo Muhidini Maalim Gurumo mwaka 1990.

JINA LA DOKTA

Watu wengi hawafahamu kwanini Mabela alipewa jina la Dokta na wengine wanataka kujua jina hilo lilitokea wapi.

“Mashabiki wa bendi yangu ndio walionipa jina la Dokta. Ilikuwa baada ya kuondoka kwa Bartazali. Niliweza kufanya kazi nzuri ndipo wakaamua kunipachika jina hilo kwa sababu nilitibu lile pengo lake alipohama bendi,” anasema.

MTUNZI MZURI TU

Pamoja na kutovuma sana katika utunzi, Mabela ni mmoja kati ya wanamuziki wenye tungo nzuri tangu bendi hiyo ikitumia jina la Nuta hadi Msondo Ngoma.

“Nimetunga nyimbo nyingi sana, nyingine hata sizikumbuki kwa kweli,” anasema na kujaribu kukumbuka chache kama vile Kifo cha Baba, Nisingekukimbia na Hebu Sikia.

KWANINI HAKUHAMA MSONDO?

Swali kubwa ambalo wengi wanajiuliza kwanini Mabela ameweza kudumu kwa bendi hiyo kwa miaka 45.

Amewezaje kudumu huku wenzake wakichukuliwa na kujiunga na bendi pinzani hususan Mlimani Park?

“Kwa kweli walikuwa hawanifuati kunishawishi kuhama kwa sababu walikuwa wanajua sitakubali kuondoka kwenye bendi hii,” anasema na kuongeza:

“Wanamuziki wengi walikuwa wanafahamu uwezo wangu na ushawishi niliokuwa nao katika bendi, hivyo nilikuwa na msimamo wa kuijenga bendi kila ilipobomoka.”

ALIMVUA DEDE SARE YA BENDI?

Mwandishi wa makala haya alimtaka Mabela kuweka wazi kuhusu tukio la kutibuana na mwimbaji wao wa zamani, Shaban Dede mwaka 1982 na kufikia kumvua sare ya bendi ya Juwata Jazz.

“Katika muziki kukorofishana na kufiwa ni vitu vya kawaida sana, kuna mambo mengi yanatokea,” anasema Mabela na kukataa kuingia kwa undani juu ya suala hilo.

Mabela alizaliwa Ujiji, Kigoma mwaka 1945 na amefanikiwa kupata watoto 11 lakini mwenyezi Mungu amemchukua mmoja na kubaki na watoto 10.

Advertisement