Asimulia mpambano polisi na majambazi ulivyokuwa

Muktasari:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna amesimulia jinsi alivyowaongoza askari wake katika mapambano kuwaua watu saba wanaotuhumiwa kwa ujambazi usiku wa Alhamis.

Mwanza. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna amesimulia jinsi alivyowaongoza askari wake katika mapambano ya dakika 45 na kufanikiwa kuwaua kwa kuwapiga risasi watu saba wanaodaiwa kuwa majambazi.

Mapambano hayo ya kurushiana risasi yalitokea saa 4:00 usiku wa kuamkia jana katika mtaa wa Ihushi kata ya Kishili jijini Mwanza, ambapo askari mmoja alijeruhiwa kwa risasi kwenye mkono wa kushoto na hali yake inaelezwa kuwa inaendelea vizuri.

Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio, Kamanda Shanna alisema kabla ya makabiliano hayo, polisi walimtia mbaroni mmoja wa watuhumiwa hao aliyemtaja kwa jina la Hashim Abas (48) ambaye aliwaongoza askari hadi kwenye maficho yao.

“Baada ya kufika kwenye maficho yao, marehemu Abas alitoa ishara kwa wenzake kwa kutamka neno ‘shemejiii’ ndipo wenzake walipoanza kuwashambulia polisi kwa risasi. Tulijibu mapigo na kuwauwa watatu waliokuwa wamejificha eneo moja,” alisema.

Alisema polisi wakitumia medani za kivita waliwaandama watuhumiwa wengine watatu waliokuwa wakitimua mbio huku wakirusha hovyo risasi na kufanikiwa kuwaua.

Diwani wa kata ya Kishili, Sospeter Ndumi ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi na ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia katika eneo hilo linaloonekana kuwa maficho ya makundi ya uhalifu mara kwa mara.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella amewapongeza polisi kwa kufanikiwa kudhibiti makundi ya kihalifu mkoani humo.