Askari wa JWTZ auawa katika mapigano DRC

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania walio kwenye kikosi maalum cha kujibu mashambulizi cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC.

Muktasari:

  • Mkuu wa Majeshi nchini Tanzania (CDF) Janerali Venance Mabeyo amewataka Watanzania kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho askari wake ameuawa akiwa analinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)

Dar/Tanga. Wanajeshi saba wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wameuawa akiwamo askari mmoja wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika operesheni ya kijeshi iliyofanywa mashariki mwa nchi hiyo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa (UN), Stephane Dujarric amesema kati ya waliouawa sita  ni kutoka Malawi na askari mmoja wa Tanzania.

Askari hao waliouawa katika mapigano yaliyozuka karibu na mji wa Beni Kaskazini mwa Kivu, Mashariki mwa Congo eneo ambalo limeathiriwa zaidi na mlipuko wa homa ya ebola.

"Ripoti za awali zinaonyesha kuwa askari 10 walijeruhiwa na mmoja hajulikani aliko,” alisema Dujarric katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini New York, Marekani.

Duru za habari zinasema kikosi hicho cha kulinda amani kilikuwa katika operesheni ya kukabiliana na wapiganaji wa kundi la waasi la Allied Democratic Forces (ADF).

Taarifa zaidi zinasema walinda amani kadhaa wa jeshi la Congo nao pia wameripotiwa kuuawa au kujeruhiwa katika operesheni hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya walinda amani waliouawa na kwa serikali za Tanzania na Malawi.

Vikosi vya waasi vimekuwa vikiendesha mapigano ya mara kwa mara nchini humo na tangu mwaka 2014 vimehusika katika mauaji ya mamia ya raia na askari 15 wa UN kutoka Tanzania waliouawa Desemba mwaka jana katika wilaya ya Beni.

Leo Ijumaa Novemba 16, 2018 akiwa mkoani Tanga, Mkuu wa Majeshi nchini Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo amewataka Watanzania kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho askari wake ameuawa kwenye mapigano hayo.

Amesema tukio hilo halijalikatisha tamaa Jeshi la Tanzania bali limesababisha kutafuta mbinu nyingine za kuendesha mapambano