Hamza Kassongo akumbusha alivyotangaza tukio la Uhuru wa Tanganyika Desemba 8 na 9, 1961

Mtangazaji mkongwe nchini, Hamza Kassongo.

Muktasari:

  • Wengi wanamfahamu mtangazaji mkongwe nchini, Hamza Kassongo kupitia kipindi chake cha televisheni cha “Hamza Kassongo Hour” Huyu ndiye mtu aliyetangaza sherehe za kuikabidhi Tanganyika uhuru wake.

Wengi wanamfahamu mtangazaji mkongwe nchini, Hamza Kassongo kupitia kipindi chake cha televisheni cha “Hamza Kassongo Hour”. Ni kipindi kinachofuatiliwa na wengi kutokana na ukweli kuwa kinakutanisha wachumi, wanasiasa na wataalamu wengine kujadili masuala ya kitaifa na kimataifa na kimemuongezea umaarufu katika tasnia ya habari.

Katika kipindi hicho kinachorushwa na kituo cha Channel Ten kila Jumapili saa 3:00 usiku, mara nyingi Kasongo huonekana akiwa amevalia tai ndogo au bow tie, wakati mwingine pamoja na mikanda maarufu ya cross belt..

Huyu ndiye mtu aliyetangaza sherehe za kuikabidhi Tanganyika uhuru wake.

Leo wakati Watanzania wakiadhimisha miaka 57 ya uhuru, Kassongo naye anaadhimisha miaka 57 ya kuweka historia ya kutangaza wakati bendera ya Tanganyika ikipanda saa 6:00 usiku na kushusha bendera ya koloni la Waingereza.

Kassongo alikuwa mmoja wa watangazaji wa Shirika la Utangazaji la Tanganyika tangu mwishoni mwa miaka ya 50.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Kassongo anaeleza maandalizi ya kupata uhuru yalivyokuwa hadi siku ilipofika. Endelea…

Swali: Unakumbuka nini siku chache kabla ya Tanganyika kupata uhuru na hadi siku ile ya uhuru wenyewe?

Jibu: Mimi nilipata bahati. Kulikuja kundi kutoka (Shirika la Utangazaji la Uingereza) BBC kutusaidia kwa sababu walikuwa na uzoefu wa Ghana na Nigeria na nchi za Jumuiya ya Madola zilizopata uhuru kabla yetu.

Kwa wale wasiofahamu, TBC yetu sisi ilikuwa ni shirika linalojitegemea. Serikali ndiyo ilikuwa inawajibika kutupa pesa, lakini tulikuwa huru kabisa kusema chochote tulichoona dhidi ya Serikali. Waliokuwa wakitusimamia ni Baraza la Magavana.

Hiyo miezi sita kabla ya uhuru nilipewa jukumu la kutembelea nchi nzima au kampuni kubwa ili kuuliza, baada ya uhuru, wakati nchi inaendeshwa na Mwafrika, nini mustakabali wao?

Kwa hiyo nikaenda kwa wakulima wa kahawa Moshi, nikaenda Iringa kwa wakulima wa Tumbaku. Hapa Dar es Salaam nikatembelea kampuni kama Sigara, Bata (viatu) bia, kampuni na bima.

Wiki moja kabla ya Desemba 9, kulikuwa na shughuli nyingi, kama vile kufungua baraza jipya na ndipo familia ya Karimjee ikatoa lile jengo kama zawadi kwa Tanganyika.

Inaendelea UK 22

INATOKA UK 23

Tarehe 8, 1961 yenyewe ndiyo ilikuwa kilele cha shughuli. Mimi nilikuwa mtangazaji kati ya watangazaji wawili. Mwenzangu alikuwa Salim Seif Nkamba tukimwita Mjomba wakati huo akipigana ngumi. Watangazaji wengine kama kina David Wakati walikuwa na majukumu mengine.

Swali: Sasa katika siku yenyewe ya Desemba 9 hali ilikuwaje?

Jibu: Barabarani huko nadhani miti ilikosa matawi, maana watu chungu nzima walikata matawi, bendera za Tanu zilikuwa hazitoshi na hakukuwa na bendera za Tanganyika. Kwa hiyo watu wakawa wanashika majani kusherehekea.

Watu walitoka Mwananyamala, sijui Kunduchi walitoka kwenda kusherehekea.

Sisi tuliokuwa zamu, tulikwenda mapema kidogo saa mbili usiku wa Desemba 8 na tulikuwa chumba kimoja na chumba kingine kulikuwa na watagazaji wa BBC waliokuja kushirikiana na sisi.

Kazi yetu kubwa ilikuwa ni kueleza kinachotokea pale, kama ngoma za utamaduni, bendi ya Polisi na mengineyo.

Mimi sasa nilipata bahati maalumu kwamba kuanzia saa 5:30 usiku ndiyo nilikuwa nimeshika zamu. Nikaeleza yanayotokea; kwanza ilikuwa ni kwenda Mlima Kilimanjaro ambapo Luteni Alexander Nyirenda kutoka Kings African Riffles (KAR) akapanda mlima.

Kama mtakumbuka Mwalimu Nyerere alisema akaweke mwenge juu ya kilele cha mlima Kilimanjaro, ili utoe matumaini. Huo ndiyo ulikuwa msimamo wetu kwa sababu uhuru wetu bado haujakamilika kama Afrika bado haijawa huru.

Jambo la pili lilikuwa ni kumwona mgeni wa heshima mme wa Malkia pamoja na Waziri Mkuu Mwalimu Julius Nyerere.

Swali: Hapo umezungumzia tukio la Nyirenda kupanda Mlima Kilimanjaro na wewe ulikuwa Dar es Salaam, uliwezaje kulitangaza wakati ule?

Jibu: Ilikuwa ni changamoto ya hali ya juu sana, maana yake ninyi wakati huu mna bahati sana, unashika simu yako unaweza kurekodi na kuandika. Sisi wakati ule tulikuwa tunatumia ‘typewriter’, haina umeme wala nini.

Sasa ilipofika kutangaza hapo, tulikwenda Posta, chumba cha kurushia matangazo yao. Tukawaomba watupe mawasiliano kati yetu sisi na Moshi, ili tuzungumze na Nyirenda kutoka juu ya Mlima Kilimanjaro.

Kwa hiyo tuliweka mitambo kutoka uwanja wa Taifa kwenda kwenye chumba maalumu (control room), kisha matangazo yanakwenda Posta, yakitoka Posta yanakwenda Moshi.

Moshi pale tulikuwa tunatumia simu ya upepo ambapo Jeshi la KAR la Kenya waliweka simu ya upepo kuzungumza mlimani.

Nyirenda ndiye aliyesoma yale maneno na akaeleza jinsi alipofika hapo mlimani kwamba alichukua siku nne na akaeleza baridi ilikuwa kali sana, akaeleza walikuwa wangapi na walipata madhila gani.

Akasema kabisa sasa nimefika hapa inakaribia saa 6:00 usiku nimewasha Mwenge wa Uhuru na nimeuweka juu ya Mlima Kilimanjaro kama nilivyotumwa na Waziri Mkuu Nyerere.

Swali: Sasa usiku huo ndiyo ukaishia hivyo.. Je, siku yenyewe ya Desemba 9 , 1961 hali ilikuwaje? Mwalimu Nyerere ndiye aliyetangulia kufika uwanjani?

Jibu: Hapana, walikwenda pamoja, ilikuwa saa 6:00 usiku. Kwanza kulikuwa na kubadilishana bendera na wakati ule bado Jeshi lilikuwa ni la Uingereza la KAR, japo wakati huo pia kulikuwa kumeshaanzishwa Tanganyika Riffles. Kwa hiyo kukawa na watu wanne huku wakiwakilisha Uingereza na wengine wanne huku wakiwakilisha Tanganyika, japo wote walikuwa Watanganyika.

Baada ya kubadilisha bendera, ukapigwa wimbo wa Uingereza wakati bendera inashushwa na kupigwa wetu ndiyo bendera yetu ikapandishwa. Hapo tena hata ungezungumza na mtu sikioni asingekusikia, maana kulikuwa na kelele kubwa. Maana hata huko nje meli zilipiga honi na magari, ilikuwa furaha kubwa.

Mchana ule wa Desemba 9, mimi na Salim Nkamba tulikwenda kupumzika, lakini jioni yake tulirudi na kulikuwa na mechi ya mpira wa miguu kati ya Tanganyika na Kenya.

Matokeo yalikuwa 2 kwa 1, sasa sijui tuliwafunga au walitufunga. Watu wote 24 waliokuwa pale hakuna hata mmoja aliyevaa viatu, wengine wamejifunga vitambaa na wengine bendeji.

Usiku wengine ndiyo walifaidi kwani viongozi walikwenda kusakata dansi.

Swali: Unawakumbuka mawaziri waliokuwepo wakati ule wa uhuru?

Jibu: Nawakumbuka mawaziri wachache tu walikuwa wamevaa suti, wengi walivaa mgolole. Namkumbuka Rashid Kawawa alivaa mgolole, Job Lusinde alivaa suti, Oscar Kambona alivaa suti, Mbunge wetu wa Kinondoni, Dereck Bryceson aliyekuwa Waziri wa Kilimo naye alivaa suti, Ernest Veze alivaa suti nadhani na Chief Abdallah Fundikira naye alivaa mgolole. Sikumbuki Said Tewa alivaa nini.

Kuvaa mgolole ilikuwa kama ishara ya kuachana na ukoloni, lakini Waziri Mkuu Nyerere alivaa suti.

Swali: Sasa tukirejea kwenye historia yako, baada ya pale uliendelea na kazi TBC hadi lini?

Jibu: Baada ya uhuru ile Desemba 9, 1961 sikukaa sana, Januari 22, 1962 nilikwenda Uingereza BBC ambako nilikaa miaka mingi mpaka 1965 nikarudi.

Mwaka huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, marehemu Paul Sozigwa, wakati huo Waziri alikuwa Hasun Makame kutoka Zanzibar.

Sozigwa alitangaza akasema kwamba kuanzia Julai TBC itakuwa Radio Tanzania. Alipoulizwa maana yake nini akasema maana yake sasa mtakuwa chini ya Serikali. Kwa hiyo sasa mishahara yetu haitakuwa juu tena bali itakuwa P1, P2 kama ya Serikali.

Itaendelea…