Kampuni kuanza kuhifadhi maiti bure

Moshi. Katika kurahisisha shughuli za mazishi, wakazi wa Moshi sasa wataweza kuhifadhi bure maiti za wapendwa wao iwapo wataingia katika makubaliano na wauzaji majeneza.

Hatua hiyo inakuja baada ya kampuni ya Goodmark Funerals Directors ya mjini hapa kuanzisha huduma ya kuuza kwa bei nafuu majeneza, iwapo mteja atanunua kabla ya kifo chake au cha mpendwa wake.

Huduma hiyo ya aina yake, pia itahusisha kurahisishwa kwa shughuli za kufunika kaburi ambazo huchukua muda mrefu iwapo waombolezaji wanatumia njia ya kawaida ya kuchanganya zege kwa ajili ya kupata mfuniko wa kaburi.

Mkurugenzi wa Goodmark, Maximillan Siraki aliiambia Mwananchi kuwa wako katika hatua ya mwisho ya kuanza ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti.

“Watu watakaonunua vifurushi vya bidhaa zetu, watapewa ofa ya kulaza mpendwa wao bure kwa siku kwa siku tatu,” alisema Siraki.

“Tutakuja na package (kifurushi) kama vilivyo vifurushi vya simu. Tutatengeneza kifurushi ambacho ni bei fulani. Tunajaribu kufanya bei ya mazishi iwe rahisi maana uchumi sasa ni ngumu kidogo.

“Unajua kitu muhimu ni marehemu anaondokaje duniani. Hivyo vitu vingine kama vyakula sio muhimu sana. Kitu muhimu ni kile marehemu anatumia kama jeneza na usafiri.

“Watu wengi huwa wanaangalia watu watakula nini lakini hivyo havimhusu marehemu. Marehemu hatakaa kwenye kiti wala hatahitaji tent (turubai). Marehemu atahitaji jeneza zuri.”

Alisema mahitaji muhimu ya maiti ni usafiri wa kumtoa hospitalini kwenda kanisani au nyumbani, mashine ya kumshusha kaburini na kuzika.

Jamii iliwatenga mwaka 1996

Ubunifu wao umepitia katika kipindi kigumu tangu walipoanza mwaka 1996 kabla ya jamii kuikubali.

“Tulikuwa wa kwanza kwanza miaka ile ya 1990 kuanza kutengeneza majeneza kama biashara katika mkoa huu na wakati tunasajili tukagundua ni kampuni ya kwanza kusajiliwa Brela,” alisema Siraki.

“Kwanza jamii ilichukulia vibaya. Watu waliona kama tunataka wafe. Tulipata changamoto kubwa mpaka kutengwa na jamii.

“Ukienda kukodi nyumba ni lazima ueleze aina ya biashara unayotaka kuifanya kwa hiyo ukishasema tu nataka kuuza majeneza duh hapohapo mwenye nyumba anakataa.”

Alimshukuru mmiliki wa eneo lao la sasa akisema aliwakubalia kuendesha biashara kwake.

“Unaweza kuona jinsi gani ilikuwa kitu kigeni,” alisema.

“Kwa sababu tulijua hatufanyi kosa wala hatujakiuka desturi yetu, tuliendelea na polepole walianza kununua. Sasa hivi maeneo yanayouza majeneza ni mengi karibu kila mahali.”

Katika barabara ya kuelekea KCMC, wauzaji majeneza takriban 20 wamepanga kwenye eneo hilo, wakiwa na lengo la kupata wateja kirahisi karibu na hospitali hiyo kubwa Kaskazini mwa Tanzania.

Idadi yao imefanya biashara hiyo kuwa ngumu kiasi cha kila mmoja kubuni mbinu ya kuvutia wateja.