‘Kopeni mkuze mitaji yenu’

Meneja Masoko wa Vodacom, Noel Mazoya  (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Uzinduzi rasmi wa Promosheni iliyopewa jina la Shinda na  M-PAWA. Watatu (wapilikulia) Mkurugenzi  Idara  Wateja binafsi na Masoko wa Benki ya Biashara Afrika CBA Julius Konyani ambae amemuwakilisha Mkurugenzi  Mkuu wa Benki hiyo,   Wengine  ni Mwakilishi kutoka Bodi ya Michezo ya kubahatisha  Jehud Ngolo pamoja na Sophet Mafuru kutoka SMSRTCODES LTD hafla hiyo imefanyika leo kwenye ofisi za benki hiyo jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Watanzania wametakiwa kutumia fursa za mikopo vizuri kwa kukuza mitaji yao ya biashara, bila kusahau wajibu wa kuirejesha kwa wakati.

Wito huo ulitolewa jana wakati wa uzinduzi wa promosheni ya M-Pawa inayofanyika nchini kwa ushirikiano kati ya Benki ya CBA na kampuni ya simu ya Vodacom.

Promosheni hiyo inayotekelezwa na Vodacom na CBA, inalenga kutoa fursa kwa washindi 200 kuongezewa mara mbili ya akiba zao kila wiki na wengine 15 watakaoweza kurudisha mkopo kabla ya siku 30 kujinyakulia Sh100,000 kila mmoja.

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa CBA, Julius Konyani alisema wametoa motisha hiyo ili kuwahimiza wateja kukopa kwa ajili ya kukuza mitaji yao kibiashara na pia kuwajengea utamaduni wa kulipa kwa wakati.

Konyani alisema katika promosheni hiyo itakayofanyika hadi katikati ya Desemba, watatoa kitita cha Sh10 milioni na bajaji tano kwa washindi wa droo kubwa ya mwisho.

Alisema hizo ni jitihada za benki hiyo na Vodacom kutaka kuleta mwamko wa kifedha na kuwahimiza Watanzania kuwa na tabia ya kuweka akiba, kukopa kwa ajili ya maendeleo na kuwajengea utamaduni wa kuirejesha kwa wakati.

Naye meneja masoko wa Vodacom huduma za fedha, Noel Mazoya alisema mteja anapokopa na kurejesha kwa wakati, inampa fursa ya kuomba tena mkopo na kuongeza kiwango cha kukopa.