Majaliwa atoa pongezi jimboni kwake.

Muktasari:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kwa kushika nafasi ya kwanza katika matokeo ya mtihani wa kumaliza darasa la saba kwa mkoa wa Lindi mwaka huu huku kitaifa wakishika nafasi ya 84.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kwa kushika nafasi ya kwanza katika matokeo ya mtihani wa kumaliza darasa la saba kwa mkoa wa Lindi mwaka huu.

Majaliwa ambaye aliambatana na mke wake ametoa pongezi hizo leo Jumapili, Novemba 18, 2018 katika mkutano wa kuwapongeza walimu wa wilaya ya Ruangwa na baadhi ya wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka huu.

Amesema matokeo ya mwaka jana halmashauri ya wilaya ya Ruangwa ilishika nafasi ya tano kimkoa na kitaifa ilikuwa nafasi ya 141, ambapo kwa mwaka huu imepanda na kuwa nafasi ya kwanza kimkoa na kitaifa nafasi ya 84.

Majaliwa ambaye ni mbunge wa Ruangwa kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Ruangwa wametoa zawadi mbalimbali kwa kata tatu bora zilizofanya vizuri, shule 10 bora, walimu ambao wanafunzi wao wamepata daraja ‘A’ katika masomo mbalimbali wanayofundisha pamoja na wanafunzi 10 bora.

Miongoni mwa zawadi hizo ni pamoja na fedha taslimu, kompyuta kwa ajili ya matumizi ya shule zilizofanya vizuri, ikiwa ni kichocheo cha kuongeza  bidii ili mwakani wapate matokeo mazuri zaidi.

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa aliupongeza uongozi wa mkoa wa Lindi kwa mikakati waliyoiweka kwa ajili ya kuboresha elimu, ambayo imesababisha kupatikana kwa matokeo hayo mazuri.

“Nawapongeza kwa sasa mimi kitaaluma ni mwalimu hivyo nafahamu ili mwanafunzi apate matokeo mazuri ni lazima mwalimu afanye juhudi kubwa zitakazomuwezesha mwanafunzi kufaulu masomo yake,” alisema Mama Majaliwa.

 

Amesema matokeo mazuri ya wanafunzi ndiyo yatakayowafanya walimu wafurahi. “Matokeo haya yasiishie hapa mwakani tuongeze bidii tuweze kupata matokeo mazuri zaidi yatakayotuwezesha kushika nafasi ya kwanza Kitaifa.”

Kwa upande wake ofisa Elimu Msingi wa wilaya ya Ruangwa, Selemani Mrope amesema kuanzia mwaka 2015 hadi 2017 hali ya ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba haikuwa nzuri kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya utoro.

Mrope ametaja sababu nyingine kuwa ni walimu kutowajibika ipasavyo, ufuatiliaji na usimamizi duni wa taaluma shuleni, ambapo viongozi wengi wa shule na kata walishindwa kusimamia ipasavyo majukumu yao na kuwaacha walimu wafanye kazi kwa mazoea.

 “Wazazi wengi kukosa kuwajibika ipasavyo katika elimu ya watoto wao na kuona elimu haina maana kwao na kushindwa kuwahimiza watoto kwenda shule na kusababisha utoro huku wengine wakidiriki kuwashawishi watoto wao wafanye vibaya kwenye mitihani yao,” amesema