Mjane arithi kazi ya mume kung’arisha viatu mtaani

Mkazi wa Ichenjezya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Ester Mtafya akipiga viatu rangi. Picha na Stephano Simbeye

Muktasari:

Ester Mtafya, mjane, mkazi wa Ichenjezya wilayani Mbozi mkoani Songwe,  amejizolea sifa tele kwa umahiri wake wa kung’arisha viatu kiasi cha kuwavutia watu wengi

Mbozi. Katika mazingira ya kawaida imezoweleka kuwa kazi ya kusafisha viatu (shoe shine) hufanywa na wanaume, lakini ni tofauti kwa Ester Mtafya, mjane, mkazi wa Ichenjezya wilayani Mbozi mkoani Songwe.

Ester amejizolea sifa tele kwa umahiri wake wa kung’arisha viatu kiasi cha kuwavutia watu wengi kumpelekea viatu vyao.

Katika mahojiano na Mwananchi, mjane huyo anasema licha ya kuipenda kazi yake ambayo inamsaidia kulea na kusomesha watoto wake wanne alioachiwa na mumewe, Benny Mwajeka, pia imemfanya kutokuwa na muda wa kupoteza katika makundi yasiyo na maana kama ilivyo kwa baadhi ya wanawake.

“Namshukuru Mungu kwa kunipa ujasiri wa kufanya kazi hii, imenisaidia kupata kipato cha kuendesha maisha yangu ya kila siku, sina shughuli nyingine inayoniingizia kipato zaidi ya hii,” anasema mjane huyo ambaye mumewe alifariki dunia 2015.

Anasema awali mumewe ndiye alikuwa akifanya kazi hiyo, lakini baadaye alianza kumlazimisha naye ashiriki hasa wakati alipopata dharura.

Jambo hilo halikumfurahisha na kumfanya akubali kwa shingo upande kutokana na kuwa alifahamu kwamba kazi kama hizo wanaume ndio huzifanya.

“Mwanzoni nilikuwa naona aibu na woga kwa kuwa wanawake wenzangu walikuwa wananicheka kuwa nafanya kazi ya wanaume, hata hivyo niliendelea kuifanya kwa kupokezana na mwenzangu (mume wangu), kama yeye akija asubuhi, mimi nilikuja jioni. Tuliendelea kubadilishana hivyo mpaka nikaanza kujifunza kushona viatu.”

Ester anasema kadri alivyozidi kuifanya kazi hiyo kwa karibu na mumewe, aliendelea kujifunza vitu vingi ikiwamo maeneo yanayouzwa viatu kwa bei nzuri.

Anasema licha ya kufanya kazi hiyo, lakini pia kwa sasa amefanikiwa kupata mtaji uliomwezesha kuanza kuuza viatu vya mitumba.

Wateja na changamoto

Akizungumzia wateja wake, Ester anasema asilimia kubwa ni wanaume.

Anasema katika utendaji kazi hajawahi kukumbana na changamoto kubwa, isipokuwa zile za kifamilia.

“Hakuna changamoto ninayopata toka mamlaka za utawala, bali changamoto kubwa ni jinsi gani naweza kuishi na watoto wangu. Hata hivyo najitahidi kukabiliana nayo,” anasema.

Mjane huyo anatoa wito kwa wanawake wenzake kutochagua kazi ya kufanya, badala yake wafanye shughuli yoyote halali itakayowapatia kipato.

Wateja wanavyomkubali

Vicent Nelson, mmoja wa wateja wanaompelekea viatu Ester kwa ajili ya kuvisafisha na kushona, anasema alianza kumhudumia tangu alipokuwepo mumewe na hata alipofariki ameendelea kuwa mteja wake kutokana na kuridhishwa na kazi anayoifanya.

“Hapa jambo la msingi si kuangalia ni nani anayefanya kazi, bali kazi inafanyika katika kiwango gani na kwa kuwa kiwango cha kazi ni kizuri tunaendelea kumuunga mkono shemeji yetu ili aendelee kulea watoto wake,” anasema Vicent.

Edina Mwaijande, anasema kitendo cha ujasiri alichokionyesha mwanamke mwenzake kinafaa kuingwa na wanawake wengine kwa kutochagua kazi.

Anasema wanaochagua kazi huishia kukusanyika wengi katika kazi moja na hivyo kunyang’anyana wateja.

“Mfano hivi sasa utakuta akina mama wengi wanauza nyanya, ndizi na mapalachichi pale stendi kuu hali inayowapunguzia wateja wakati wangeweza kutawanyika kwa kubuni miradi mingine hata hii inayofanywa mara nyingi na wanaume ili wajipatie wateja,” anasema Edina.

Kaimu ofisa maendeleo ya jamii Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Merania Kwai anasema wapo wanawake ambao wanafanya kazi zilizozoweleka kufanywa na wanaume, lakini wanahitaji kuongezewa nguvu na hamasa ili watambue kuwa kazi yoyote inaweza kufanywa bila kujali jinsia.