TIC yalia na sheria ya uwekezaji nchini

Katibu mtendaji wa kituo hicho, Geofrey Mwambe

Muktasari:

Upungufu uliopo kwenye sheria ya uwekezaji unasababisha Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) umeshashajadiliwa na kinachosubiriwa ni mabadiliko hayo kupelekwa bungeni.

Dar es Salaam. Upungufu uliopo kwenye sheria ya uwekezaji unasababisha Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) kukosa mamlaka ya kufuatilia na kuratibu utekelezaji wa uwekezaji wa miradi ya madini, mafuta, gesi na kemikali hatari.

Akizungumza wakati wa kutoa tathmini ya utendaji wa miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano jana, katibu mtendaji wa kituo hicho, Geofrey Mwambe alisema tayari suala hilo limeshajadiliwa na kinachosubiriwa ni mabadiliko hayo kupelekwa bungeni.

Alisema kutokana na sheria iliyopo, kituo hicho kinahusika na miradi yote ya uwekezaji isipokuwa ya madini, gesi, mafuta na kemikali hatari jambo ambalo wanataka lifanyiwe marekebisho ili kuiwezesha TIC kuwa na takwimu na taarifa za uwekezaji wote.

Kingine kinachotakiwa kurekebishwa ni kigezo cha mtaji wa mwekezaji kusajiliwa TIC kwani kwa sheria ya sasa, mwekezaji wa ndani anatakiwa kuwa na mtaji wa Dola za Marekani 10,000 (Sh23 milioni) za Marekani wakati mwekezaji mtaji wake unapaswa kuwa Dola500,000.

“Tunataka tuongeze wigo wa uwekezaji, inawezekana wapo watu wana fedha nyingi lakini hazijafika kiwango hicho wanashindwa kuja kusajiliwa na TIC, sasa sheria ikibadilishwa hawa wote tutawaratibu na kufuatilia utendaji wao,” alisema Mwambe.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano, kituo hicho kimeendelea kuratibu, kushawishi na kuhamasisha uwekezaji na kuifanya Tanzania kuongoza nchi za Afrika Mashariki katika uwekezaji.

Kwa mujibu wa Mwambe, jumla ya miradi 905 ya uwekezaji imesajiliwa nchini katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa Rais John Magufuli, yote ikiwa na thamani ya Dola13.2 bilioni za Marekani.

Kati ya miradi hiyo, 307 ni ya Watanzania, 319 ya wawekezaji kutoka nje na 277 ni miradi ya ubia kati ya Watanzania na wageni huku 478 ni ya viwanda vilivyokidhi vigezo vya kusajiliwa na kituo hicho na uwekezaji mkubwa ukifanywa na nchi ya China.

Mwambe alieleza kuwa uwekezaji huo ukifika miaka mitano, utakuwa umetoa ajira za moja kwa moja 115,055.