Tamisemi yabaini asilimia 14 ya walimu ni watoro

Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara

Muktasari:

  • Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara alisema licha ya Taarifa zinaonyesha asilimia 14 ya walimu hawapo kabisa, lakini mwisho wa mwezi wanadai mishahara, pia asilimia 50 ya walimu waliopo shuleni, ufundishaji wao si wa kuridhisha.

Dodoma. Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)imesema asilimia 14 ya walimu nchini ni watoro.

Akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa), naibu waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara alisema licha ya taarifa kuonyesha idadi hiyo hawapo shuleni, walimu wakuu hawatoi taarifa juu ya utoro huo.

“Taarifa zinaonyesha asilimia 14 ya walimu hawapo kabisa, lakini mwisho wa mwezi wanadai mishahara. Hawa ndiyo wanachangia upungufu wa walimu shuleni,” alisema Waitara.

Alisema wakati walimu hao wanawajibishwa kwa utoro na walimu wakuu nao watawajibika kwa kutotoa taarifa na kuacha walimu hao kulipwa mishahara ya bure.

Alisema asilimia 50 ya walimu waliopo shuleni, ufundishaji wao si wa kuridhisha. “Lazima kurudisha nidhamu halisi ya walimu tunaanzaje, lazima tuanze na hawa walimu watoro ambao hawaonekani shuleni kabisa,” alisema.

Pia, Waitara alisema fedha zaidi ya Sh1.1 bilioni zilizokuwa za mpango wa kuboresha elimu (Equip) zilizotolewa katika halmashauri za mikoa tisa nchini, zimepelekwa katika matumizi mengine. “Wakati uamuzi unafanyika ziende kwenye shule, hazikufanyika bahati mbaya kuna case study (mifano) nyingi ambazo zilifanyika zikionyesha kuwa fedha zilikuwa zinachelewa kwa hiyo tukasema ziende moja kwa moja site (shule),” alisema.

Alizitaja halmashauri hizo kuwa ni Kigoma Sh345.5 milioni, Lindi (Sh40 milioni), Butiama (Sh417 milioni), Liwale (Sh160.3 milioni), Mpwapwa (Sh95.5 milioni), Chemba (Sh32 milioni) na Bahi Sh86.3milioni na kwamba wamewaandikia barua wakurugenzi kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua kwa kutumia fedha za miradi ya elimu kinyume na maelekezo.

Alisema wataangalia pia, wakuu wa shule ambao hawakuchukua hatua yoyote licha ya fedha kubadilishwa matumizi kinyume na maagizo ya Tamisemi.

“Fedha zinakuja kwako, halafu mkurugenzi anakwambia ubadili matumizi unakubali. Tunaposhughulika huyu mkurugenzi na mkuu wa shule utawajibika kwa sababu na wewe ulikuwa na uwezo wa kukataa,” alisema.

Alisema watamsamehe mwalimu mkuu, ambaye fedha zimetumika kinyume na maelekezo na alitoa taarifa Tamisemi na haikushughulikiwa.

Alisema sambamba na kuwataka wajieleze pia wamewataka wakurugenzi hao kurejesha fedha hizo walizozitumia kinyume na maelekezo.

Waitara aliwataka walimu ambao hawakupewa fedha za posho na nauli kwa ajili ya mkutano huo kwenda kwa wakurugenzi wao mara watakapomaliza mkutano kuzichukua.

Agizo hilo lilitokana na maelezo yaliyotolewa na mwenyekiti wa Tahossa, Vitalis Shija aliyesema ingawa wizara imeagiza wakurugenzi wa halmashauri kutoa nauli na posho kwa wakuu wa shule, baadhi hazijafanya.

Alizitaja halmashauri hizo kuwa ni Moshi, Chato na Nkasi jambo ambalo limewafanya wakuu hao kujigharamia wenyewe usafiri.