Uhuru ulindwe na mifumo isiyokiuka haki kwa raia

Marais wastaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wakibadilishana mawazo wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru, kwenye  Uwanja wa Jamhuri,  mjini Dodoma jana. Picha na mpigapicha wetu

Muktasari:

Leo tukiwa tunatimiza miaka 57 ya Uhuru wa Tanganyika, upo wajibu wa jumla kwamba mifumo yenye kuratibu Uhuru wa watu lazima iwe imara ili kuhakikisha Mtanzania anakuwa huru na anaonekana yupo huru.

Leo ni miaka 57 tangu Tanganyika ilipopata uhuru. Kumbukumbu kubwa ya siku hii ni jinsi ambavyo waasisi wa nchi walivyovuja machozi, jasho na damu ili kulifanya nchi ya Tanganyika iwe huru kisha watu wake wawe huru.

Kila inapofika Desemba 9 kama leo, inatakiwa siyo tu kusherehekea uhuru kwa kupiga mizinga ya kijeshi na kufanya maonesho ya gwaride, bali tukumbuke nyakati za wazee wetu kujinyima, kuyatoa sadaka maisha yao ili hatimaye nchi iwe huru.

Kuwaombea pumziko lenye usalama waasisi waliotangulia, kisha mmoja mmoja waliobaki kuendelea kuwaenzi na kuwatunza, ndiyo ‘tambiko’ kuu la nchi yetu, lakini zaidi ni ishara ya shukurani kuwa tunavyoona vinaelea leo viliundwa. Uhuru tunaojidaia leo wazee wetu waliubebea gharama ya hali ya juu.

Uhuru unaotakiwa

Maneno mawili ya Kiingereza, “Independence” na “Freedom” yanatuleta kwenye maana moja ya Uhuru. Hata hivyo, mantiki za maneno hayo ni tofauti, lakini zinapaswa kwenda sambamba ili kudhihirisha kweli Taifa ni huru.

Independence ni Uhuru wa nchi kujiamulia mambo yake yenyewe bila kuingiliwa wala kuwa chini ya shuruti za mamlaka nyingine. Vilevile independence ni uhuru wa mtu kujiamulia mambo yake na kutokuwa tegemezi kimaisha.

Freedom ni nguvu au haki ya kutenda, kuzungumza na kufikiri kwa namna mtu anavyojisikia. Freedom pia ni hali ya mtu kutofungwa jela au kutowekwa utumwani. Utaona kuwa hapa tunazungumzia zaidi uhuru binafsi.

Kwa mantiki zote mbili, ni dhahiri kuwa Independence na Freedom kwa pamoja ndio tunapata Uhuru wa Taifa. Maana nchi inakuwa huru na watu wake wanajiona wapo huru. Kwa tafsiri hiyo ni kuwa nchi inaweza kuwa huru lakini Taifa likawa si huru.

Uhuru wa Taifa unagusa maeneo mawili; nchi na watu wake. Hivyo basi, miaka 57 baada ya Uhuru, ni uhakika kuwa nchi ni huru. Swali linakuja; Taifa lipo huru? Yaani Watanzania wana uhuru ambao wanatakiwa wawe nao. Uhuru wa Watanzania kwa makundi na mmoja mmoja katika nchi huru ndiyo tunapata Uhuru wa Taifa.

Leo tukiwa tunatimiza miaka 57 ya Uhuru wa Tanganyika, upo wajibu wa jumla kwamba mifumo yenye kuratibu Uhuru wa watu lazima iwe imara ili kuhakikisha Mtanzania anakuwa huru na anaonekana yupo huru. Hasumbuliwi katika uhuru wake. Haingii gharama yoyote kuhakikisha anakuwa huru. Hatokei yeyote mwenye kuhatarisha uhuru wake.

Ukiisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sehemu ya utangulizi kisha ibara ya kwanza mpaka ya 30, inazungumzia utu, haki na uhuru wa Watanzania. Mambo hayo matatu kwa kujumlisha na uhuru wa nchi, ndipo tunapata uhuru wa Taifa.

Hata hivyo, utu na haki haviwezi kuonekana kama watu hawapo huru. Kwa hiyo uhuru wa watu unapaswa kutangulia.

Mifumo ya uhuru

Katika nchi huru lazima kuwe na mifumo madhubuti yenye kuzuia haki za watu kupokonywa. Katiba ya nchi imetoa uhuru wa watu kwa sababu inajitambulisha yenyewe kuwa ni Jamhuri iliyo huru. Haki na utu ni alama za uhuru.

Nchi ambayo watu wake haki zao zinadhulumiwa na utu wao unatwezwa au kushushwa hadhi, maana yake hakuna mifumo yenye kulinda uhuru wa watu kupokonywa. Mwisho kabisa ni watu kujiona hawapo huru au wanaonyanyasika kwenye nchi yao. Sheria nyingi zenye kudhibiti uhuru wa kutoa maoni hazingepitishwa kama kungekuwa na mifumo madhubuti ya kuzuia haki za watu kupokonywa. Malalamiko mengi kuwa uhuru wa kutoa maoni umepokonywa ni kipimo cha mifumo iliyopo kushindwa kufanya kazi ya kuulinda uhuru wa watu.

Bunge ndicho chomo chenye wajibu wa moja kwa moja wa kupaza sauti za watu. Hata hivyo, ni Bunge hilohilo ambalo linabeba lawama kwamba linapitisha sheria ambazo zinaingilia uhuru wa watu, wakati lenyewe ndilo linapaswa kudhibiti watu wasinyimwe uhuru.

Sasa hivi kuna Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo ni wazi inakuja kuvinyima uhuru vyama vya siasa. Tayari kuna Sheria ya Makosa ya Mitandao, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari na kadhalika. Wingi wa sheria zenye kuubana uhuru wa watu si sifa njema, kwani ni kusababisha nchi iwe huru lakini Taifa si huru.

Mifumo ya utoaji haki lazima ijengwe kwa nidhamu ya hali ya juu. Mahakama zikichezewa na kufanya wenye nguvu kuamua watu wasio na hatia kwenda jela na wenye hatia kupeta mitaani, huko ni kuvuruga uhuru wa Taifa.

Sherehe za miaka 57 ya uhuru ziendane na kuboresha mifumo ya kudhibiti wanyonge kudhulumiwa. Ziwadhibiti pia watu wenye kutumia mamlaka zao vibaya kukandamiza wasio na mamlaka. Taifa la watu huru ni lile ambalo hata mnyonge hana wasiwasi wa kupata haki yake pindi inapochukuliwa na mwenye nguvu.

Mwalimu Julius Nyerere alitaka uhuru ulete matumaini palipokata tamaa, upendo kwenye chuki, heshima palipo na dharau. Alitaka uhuru umfanye Mtanzania awe raia mwenye hadhi.