VIDEO: Masha alia na Serikali ndege yake kuzuiwa

Muktasari:

Mwenyekiti mtendaji wa Shirika la Ndege la Fastjet Tanzania,  Lawrance Masha amesema Serikali imemzuia kuingiza ndege za  shirika hilo ingawa ana matumaini mambo yatakuwa mazuri.

Dar es Salaam. Mwenyekiti Mtendaji wa shirika la ndege la Fastjet Tanzania, Lawrence Masha amesema Serikali imemzuia kuingiza ndege kwa ajili ya kulifufua shirika hilo, lakini anaamini baada ya sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya huenda mambo yakawa tofauti.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Uchukuzi), Leonard Chamuliho aliliambia Mwananchi jana kuwa bado shirika hilo halijawasilisha malalamiko yoyote wizarani ambayo ni kikwazo kwao kufanya shughuli zao.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Hamza Johari aliliambia Mwananchi jana kuwa, leo atazungumza na wanahabari ili kutoa ufafanuzi wa mambo yote yanayoendelea baina ya mamlaka hiyo na Fastjet. “Mambo yanayozungumzwa hata katika mitandao ya kijamii ni mengi, niko safarini natoka Dodoma kuja Dar es Salaam, kesho (leo) saa nne asubuhi nitazungumza na wanahabari kuyatolea ufafanuzi,” alisema Johari alipoulizwa kuhusu ushirikiano ambao TCAA inautoa kwa Fastjet.

Madai ya Masha

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam, Masha alisema Serikali haimpatii ushirikiano wa kutosha kuifufua Fastjet kiasi cha kumzuia kuingiza ndege aina ya Boeing 737-500, baada ya iliyokuwepo kuzuiwa kuruka kwa madai kuwa inapata hitilafu mara kwa mara na shirika hilo halina meneja mwajibikaji.

Desemba 19, akizungumza katika kipindi cha 360 kinachorushwa na televisheni ya Clouds, Masha alisema ndege hiyo ingefika nchini Desemba 22, lakini hadi jana ilikuwa haijafika.

Jana alisema endapo Serikali itamruhusu ndege hiyo itafika ndani ya muda mfupi kwa kuwa kila kitu kiko tayari na safari ya kutoka Afrika Kusini iliko hadi nchini ni saa tatu.

“TCAA inasema ili niweze kuingiza ndege hiyo nimalize kwanza madeni yote, baadhi ya madeni yanalipwa na mengine tayari yamelipwa na Fastjet Plc, mengine Fastjet Tanzania tayari tumemaliza lakini fedha imeisha,” alisema.

Masha alisema, “Fedha nyingine tulizitumia kutimiza matakwa ya mamlaka inayotusimamia, sasa wangeniruhusu nifaye kazi ili nipate fedha ya kulipa yaliyobaki.”

Alisema ndege iliyozuiwa kuja nchini imekwishalipiwa na iko tayari kuja pamoja na wafanyakazi wote wakiwamo marubani, hivyo kuzuiwa kwake ni hasara kwao.