Vikokotoo viwili kulipa mtu mmoja

Muktasari:

  • Suala la mafao limeendelea kuibua mjadala kuanzia kanuni zinazotumika katika ukokotoaji na Sheria ya Usimamizi wa Mfuko wa PSSSF ambao wanachama wake ni watumishi wa umma, taasisi na kampuni ambazo Serikali inaeleza mtumishi ambaye umri wake ulikuwa zaidi ya miaka 55 hadi Agosti Mosi atalipwa mafao kwa kutumia vikokotoo viwili.

Dar es Salaam. Suala la mafao limeendelea kuibua mjadala kuanzia kanuni zinazotumika katika ukokotoaji na Sheria ya Usimamizi wa Mfuko wa PSSSF ambao wanachama wake ni watumishi wa umma, taasisi na kampuni ambazo Serikali inamiliki zaidi ya asilimia 30.

Sheria hiyo iliyoundwa mwaka huu baada ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii, inaeleza mtumishi ambaye umri wake ulikuwa zaidi ya miaka 55 hadi Agosti Mosi atalipwa mafao kwa kutumia vikokotoo viwili.

Mfano katika pensheni ya uzee kwa watumishi wote hadi Julai 31, ambao walikuwa wanachama wa PSPF, LAPF na GEPF, pensheni yao itakokotolewa kwa fomula ya zamani ambayo ni 1/540 zidisha miezi ya utumishi zidisha mshahara wa mwisho wa mwaka.

Pia kwa pensheni hiyo, kitatumika kikokotoo kipya ambacho kinawahusu watumishi wote ambacho ni 1/580 zidisha miezi ya utumishi zidisha wastani wa mishahara ya miaka mitatu (APE).

Mafao ya mkupuo ambayo yameibua mjadala mkubwa tangu kuundwa kwa sheria hiyo yatakokotolewa kwa kutumia kikokotoo cha zamani zidisha 0.25 zidisha 15.5 jumlisha kikokotoo cha sasa zidisha 0.25 X 12.5. Na pensheni ya kila mwezi itakokotolewa kwa kutumia kikokotoo cha zamani zidisha 0.75 zidisha 1/12 jumlisha pensheni ya kikokotoo kipya zidisha 0.75 zidisha 1/12.

Mfano, mwanachama ambaye hadi Agosti alikuwa na miaka 56 mshahara wake wa mwisho ukiwa ni Sh1.268 milioni akiwa ameajiriwa mwaka 1980 wastani wa miaka mitatu ukiwa ni Sh1.178 milioni, hesabu yake itakuwa 1/540 zidisha 457 zidisha 1,268,000 zidisha 12 ambayo ni sawa na Sh 12,877,244.44 kama pensheni yake ya mwaka kabla ya Agosti Mosi.

Hivyo malipo yake ya mkupuo yatakuwa sawa na pensheni yake ya mwaka zidisha kwa 0.25 zidisha 15.5 ambayo itakuwa ni Sh49,899,322.22 na pensheni yake ya kila mwaka itakuwa Sh804,827.78 (MP1) ambayo inapatikana na kwa kutumia pesheni ya mwaka zidisha 0.75 zidisha 1/12.

Kwa mtumishi huyohuyo baada ya Agosti Mosi (fomula ya kikokotoo kipya itakuwa 1/580 x 505 x 1,178,000 x 12 ambayo ni sawa na Sh12,308,069 hivyo mafao mkupuo yatakuwa Sh38,462,715.52 ambayo ni (pensheni ya mwaka x 0.25 x 12.5 na pensheni ya kila mwezi itakuwa Sh600,979.93.

Aidha mkupuo kwa kipindi cha miaka minne baada ya Agosti Mosi utakuwa 48/505 x 38,462,715.5 ambayo ni sawa na Sh3,655,862.06 hivyo pensheni ya kila mwezi itakuwa 73,117.24 (MP2).

Mkupuo kwa kipindi cha miaka 60 utakuwa Sh49,899,822.22 kujumlisha Sh3,655,862 ambayo itakuwa Sh53,555,684.28 na pesheni ya kila mwezi itakuwa MP1 + MP2 ambayo itakuwa Sh877,945.02.