Vuai: CUF si tishio kwa CCM na haijawahi kuwa tishio

Muktasari:

  • Tangu ufanyike Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi 1995, uhusiano wa vyama vya CCM na CUF umekuwa wa vuta-nikuvute. CUF inalalamika kuibiwa kura mara zote, huku CCM ikijinasibu kupendwa na wananchi ndiyo maana imekuwa ikishinda.
  • Katika mahojiano na Mwananchi, aliyekuwa naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, pamoja na mambo mengine, anazungumzia uhusiano huo, akitamba kuwa CUF haijawahi kuwa tishio kwa CCM.

Swali: Vuai Ali Vuai, baada ya kustaafu nafasi yako ya naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, kwa sasa unajishughulisha na kazi gani?

Jibu: Kwa sasa nipo hapa ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, nikiwa mshauri wa masuala ya kisiasa. Makamu wa Pili wa Rais ndiye mtendaji mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Swali: Ikitokea ukarejeshwa kwenye nafasi ya uongozi kupitia chama chako ni jambo gani ambalo litakuwa kipaumbele chako?

Jibu: Chama chetu ni chama cha siasa, tena kilicho imara tena chenye kufuata katiba, hata hivyo sidhani kama ninaweza kurejeshwa kwenye nafasi niliyokuwa nayo au nyingine zaidi. Lakini ikitokea kurejeshwa basi hakuna kipya kwangu ambacho nitaanza nacho bali nitafuata katiba na ilani ya chama ambayo imeweka wazi nini chama au kiongozi anatakiwa kufanya kwa wanachama wake.

Swali: Kwa maoni yako unazungumziaje Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kimekuwa tishio kwa CCM kwa muda mrefu?

Jibu: Hapana, chama cha CUF hakijawahi kuwa tishio kwetu tangu kuanzishwa kwake na hadi leo hii. Na ndiyo maana tumekua tukiongoza Serikali kila baada ya miaka mitano. CUF haikuwahi kututisha na itaendelea kubaki hivyo.

Swali: Wakati wa uongozi wako kama naibu katibu mkuu CCM

Zanzibar ni changamoto gani ulikutana nazo?

Jibu: Kwanza nikiri kwamba kipindi chote ambacho nimehudumu kulikuwa na changamoto mbalim

bali zilijitokeza ingawa sitaweza kuzitaja zote. Miongoni mwa changamoto hizo ni kuwapo watu wenye shida zao, nyingine za fedha na sikuwa na uwezo wa kuzitatua, lakini nilifanya jitihada ya kuwaelekeza sehemu nyingine ambako naamini walisaidiwa.

Jambo hilo huenda wengine hawakulifurahia na ndio maana nimekuwa nikiita changamoto, kwani wengi waliamini kwamba kila anayekuja kwangu shida yake itamalizika na kuondoka.

Pili, kuna wakati tulikuwa na mtu ambaye alikuwa kiongozi wa juu kwenye chama chetu, lakini kwa kukiuka taratibu zetu za chama, vikao vyote viliamuru mwanachama huyo kufukuzwa uanachama, jambo ambalo lilikuwa tatizo kubwa kwangu.

Utakumbuka kuwa mtu huyu ambaye sitapenda kumtaja jina, alikuwa na marafiki wakubwa na wenye vyeo kwenye chama na Serikali, hivyo nilikuwa kwenye wakati mgumu sana na sitaweza kusahau.

Lakini, jambo hilo lilinifanya kuwa na msimamo na sikuyumba badala yake nilisimamia kile ambacho nimekiamini na baadaye kila mtu alifahamu ukweli.

Swali: Je, utaratibu uliotumika kukuondoa katika nafasi yako ya uongozi unadhani ulikuwa sahihi kipindi kile?

Jibu: Ndiyo, ulikuwa sahihi kwa maana chama chetu kinaongozwa na katiba na kila kitu kilifanyika kwa mujibu wa katiba. Kama suala ni nafasi ya naibu katibu mkuu, mimi sikuwa wa kwanza hapa Zanzibar, walikuapo wengi na wameondoka na kupisha wengine.

Swali: Kwa maoni yako bado unadhani wananchi wa Zanzibar wanahitaji kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK)?

Jibu: Suala hilo lina nyanja pana zaidi ambazo kila mtu ana maoni yake, kwanza nafikiri ni vyema kujua sababu ya muundo huo wa Serikali.

Ni dhahiri kuwa Wazanzibari walichoshwa na hali ya mtafaruku wa kisiasa kila mara na ndiyo maana kukaja ajenda ya mfumo huo wa SUK.

Pia, nikishukuru chama changu kwa kuniteua kuwa sehemu ya kamati ambayo ilisaidia kuwapo kwa Serikali hiyo ambayo ipo kwa mujibu wa sheria.

Lakini, licha ya kuwa matarajio ya Wazanzibari walio wengi waliamini kuwa uwepo wa SUK utazika chuki na kuendelezwa kwa umoja baina ya watu, jambo ambalo naweza sema kwa sasa ni kinyume na matarajio.

Wenzetu wa CUF miaka mitatu baada ya SUK walianza kususia baraza na hata kutoka wakati wa hotuba ya bajeti kuu ya Serikali, jambo ambalo naweza sema ndio chanzo cha kuanza kuitia doa SUK.

Watu wengi walihuzunishwa na kitendo kile kwani hakikustahiki kufanywa wakati ule ambao sote tuliamua kuwa wamoja, lakini wenzetu kumbe walibaki na ajenda zao pembeni.

Sasa tukirudi kwenye hoja ni kwamba muundo huu wa Serikali umeletwa na wananchi wenyewe kupitia kura ya maoni, hivyo wakiona wamechoshwa nao wataamua wenyewe kwa kura ileile ya maoni na sitakuwa tayari kuwasemea.

Swali: Je, unazungumziaje makundi ya makada kwenye chama chenu wanaotajwa kuwania kumrithi Dk Ali Mohamed Shein kwenye nafasi ya urais?

Jibu: Niseme kwamba jambo hilo muda wake haujafika na naamini wanaotenda hayo si wote wanania njema, lakini pia naamini wapo watu wanaweza kutumia fursa hiyo kama sehemu ya kuchafuana kisiasa.