Kitanzi kipya kwa Vyama vya siasa

Muktasari:

  • Muswada wa marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2018 umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni pamoja na mambo mengine, ukipendekeza kuongezwa kifungu kitakachomwezesha msajili wa vyama vya siasa kusitisha ruzuku au usajili wa chama atakachoona kinavunja sheria.

Dodoma/Dar. Serikali jana iliwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa unaopendekeza mabadiliko tofauti, yakiwamo ya udhibiti wa fedha za ruzuku na vyama kuingiza maudhui yatakayotangazwa na waziri.

Mapendekezo hayo pia yanampa Msajili wa Vyama vya Siasa uwezo wa kusimamisha ruzuku kwa muda atakaobainisha au kutobainisha, kuvifuta iwapo vitashindwa kukidhi utashi wa kisheria na kutoa adhabu ya faini na vifungo kwa makosa tofauti, hatua ambayo imetafsiriwa na baadhi ya wanasiasa kuwa utaua demokrasia.

“Muswada umejaa adhabu za kijinai na hivyo kufanya shughuli za vyama kuwa jinai wakati ni haki ya kikatiba,” alisema John Mrema, mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema,

“Unatumia general statements (sentensi jumuishi) kama vile gender, social inclusion, pressure groups bila ya kuyapa tafsiri ya kisheria. Unampa Msajili (mamlaka) ya kutafsiri maneno hayo kama atakavyo.”

Muswada huo umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni na mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge aliyeongoza kikao jana, alisema Spika Job Ndugai ataupangia kamati ya Bunge itakayouchambua.

Muswada huo unavitaka vyama vinavyopata ruzuku, kufungua akaunti maalumu ya fedha hizo na pia kumpa Msajili uwezo wa kusimamisha ruzuku kwa muda atakaobainisha au asiobainisha pale atakaporidhika kuwa chama kimeshindwa au hakina uwezo wa kusimamia fedha hizo.

Pia unampa waziri mamlaka ya kutengeneza kanuni za uandaaji wa taarifa za hesabu za vyama vyama na mambo yatakayojumuishwa katika katiba za vyama vya siasa.

Pia vyama havitatakiwa kufanya kazi kwa misingi ya kiharakati, kwa maana ya kushinikiza maoni ya wananchi au Serikiali kufanya jambo fulani kwa lengo fulani.

Endapo muswada huo utapitishwa kuwa sheria, chama kitakachopata hati chafu au isiyoridhisha katika ukaguzi wa hesabu zake kitazuiwa kupata ruzuku kwa miezi sita.

Vilevile, Msajili atakapotia shaka juu ya matumizi ya chama chochote, anaweza kumwomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali akifanyie ukaguzi maalumu.

Ili kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa, vyama vinatakiwa kuingiza kwenye katiba zao vipengele vya sheria ndani ya miezi sita baada ya kutolewa waraka wenye orodha ya masuala yanayotakiwa kuingizwa na kitakachoshindwa kufanya hivyo, kitakabiliwa na adhabu ya kufutwa.

Msajili pia anapewa uwezo wa kufuta usajili wa chama kitakachobainika kusajiliwa isivyo za halali.

Vikundi vya ulinzi

Muswada huo unapiga marufuku vyama kuwa na vikundi vya ulinzi vinavyofanya kazi zinazofanana na Jeshi la Polisi. Vikundi hivyo ni kama Green Guard cha CCM, Red Brigade (Chadema) na Blue Guard (CUF) na chama kitakachokiuka kipengele hicho, kitafutiwa usajili.

Kiongozi au mwanachama atakayehusika, atakabiliwa na kifungo kisichopungua miaka mitano jela na kisichozidi miaka 20 jela, unasema muswada huo.

Muswada huo pia unaweka masharti kwa mtu au taasisi inayotaka kutoa elimu ya uraia au uwezeshaji mwingine kwa vyama, kumfahamisha Msajili na kutoa sababu za ombi hilo.

“Mtu atakayekiuka kifungu hicho akipatikana na hatia atatozwa faini si chini ya Sh1 milioni na isiyozidi Sh5 milioni au kifungo kati ya miezi sita na mwaka mmoja au vyote kwa pamoja,” unaeleza muswada huo.

Msajili wa Vyama anaweza kumuagiza kiongozi au mwanachama wa chama cha siasa kumpa taarifa zozote anazohitaji wakati wowote na atakayekiuka, atakabiliwa na faini ya kati ya ShSh1 milioni na Sh10 milioni.