Wakulima Kagera wasotea malipo ya kahawa

Muktasari:

Kilio cha wakulima hao ni juu ya malipo yao kuchelewesha na malipo madogo, huku wabunge wanne kutoka mkoani humo wakitoa vilio vyao kulalamikia namna vilio vya wakulima hao vinavyoshughulikiwa

Bukoba. Baadhi ya wakulima mkoani Kagera wamesema bado wanasotea malipo ya mauzo ya kahawa, huku wengine wakihofia kushindwa kuwapeleka watoto wao shule ambao hawakuchaguliwa kujiunga na zile za Serikali.

Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Serikali ilisema zaidi ya wanafunzi 14,000 nchini hawakuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa.

Mmoja wa wakulima wanaolalamikia kutolipwa, Jasper Cronery, mkazi wa Kijiji cha Nyakibimbili alidai alipeleka tangu mwezi Julai zaidi ya kilo 300 za kahawa kwenye chama cha ushirika cha msingi kwa ahadi kuwa angelipwa baada ya siku chache, lakini amesubiri hadi sasa bila mafanikio.

Mkulima wa Kijiji cha Buhanga wilayani Muleba, Deus Robart alisema pamoja na bei ndogo ya Sh1,000 kwa kilo, bado malipo hayo hayajafanyika kwa wakulima wengi na ahadi za kulipwa zimewachosha.

Hata hivyo, bei hiyo ndogo na ucheleweshaji malipo vimewaibua wabunge wanne wa Mkoa wa Kagera wakisema mfumo mpya wa ununuzi wa zao hilo hauonekani kuwanufaisha wakulima na umekuja ghafla bila maandalizi ya kutosha.

Katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare alisema wakulima wanataka bei nzuri ya mauzo na siyo maneno matamu wanayoambiwa.

“Mkulima wa Kagera yuko sawa na aliyepo Mtwara, wapo ambao hawajalipwa mpaka leo wanataka fedha iwanufaishe na si kupigana chenga, wanatakiwa wauze bila kuwapo migogoro kama ilivyojitokeza katika msimu huu,” alisema Lwakatare.

Mbunge wa viti maalumu, Bernadetha Mushashu alisema wakulima wanapata bei ndogo huku wakitumia gharama kubwa na mbaya zaidi wengi wao hawajalipwa hadi sasa.

“Hii haiwezekani, hawa ni watu, wametumia gharama kubwa kuzalisha zao hili, kwa nini wahangaishe kulipwa fedha zao?” alihoji Mushashu.

Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate ambaye eneo lake linatajwa kukithiri kwa magendo ya kahawa, alisema kupiga marufuku uuzaji nje ya mfumo rasmi haitamsaidia mkulima kama hakuna njia mbadala za kuwasaidia.

Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa ambaye pia ni mbunge wa Karagwe alisema msimu huu umekuwa na mvurugano na kukiri kuwa kuna wakulima hawajalipwa.