15 kutoa ushahidi kesi ya Zitto Kabwe

Muktasari:

Watu 15 watatoa ushahidi katika kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge wa  Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe.


Dar es salaam. Upande wa mashtaka umepanga kuwasilisha mashahidi 15 na vielelezo vitatu zikiwemo nyaraka mbili za maandishi katika kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo)  Zitto Kabwe.

Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga ameeleza hayo leo Alhamisi Desemba 13, 2018 katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Huruma Shahidi baada ya kusoma maelezo ya awali.

Katika maelezo hayo anaeleza Oktoba 28, 2018  Zitto anadaiwa kutenda makosa hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama chake.

Inadaiwa kuwa Zitto akiwa katika mkutano huo alitoa maneno ya kuchochea chuki miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la Polisi.

“Watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi, wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya cha Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua,”  amesema Katuga akinukuu sehemu ya maneno ya Zitto aliyoyatamka katika mkutano huo.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, Zitto alikana isipokuwa jina lake na tarehe aliyokamatwa na kufikishwa mahakamani.

Wakili Katuga aliiomba mahakama kuwapa muda kwa ajili ya kuandaa mashahidi  na kesi hiyo itatajwa Januari 14, 2019 kabla yakuanza kusikilizwa Januari 29.