TCU yakunjua makucha kuvibana vyuo vikuu, kimoja chafungiwa

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa

Dar es Salaam. Wakati Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ikivionya vyuo vinavyokiuka sheria na miongozo ya utoaji wa elimu, jana ilitoa wiki mbili kuanzia Novemba 7 kwa vile vyote vinavyopaswa kuwahamisha wanafunzi kufuata utaratibu wa uhamisho na kukamilisha shughuli hiyo ndani ya wiki mbili.

Kauli hiyo ya TCU imekuja siku 13 baada ya wanafunzi 160 wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Josiah Kibira (JoKUCo) cha Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (Tuma) “kutelekezwa” katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), baada ya kusitishwa kutoa masomo na TCU na kutakiwa kuwahamishia wanafunzi wao vyuo vingine kwa gharama zao.

Katika maelekezo yake jana, TCU iliviagiza vyuo vikuu vinavyopaswa kuahamisha wanafunzi kuwasiliana haraka na vile wanavyotakiwa kuhamia, na taarifa zote zipelekwe kwenye vyuo wanakokwenda na kuwataarifu wanafunzi kuhusu kuhamia huko.

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa jana alisema hawatasita kuchukua hatua stahiki kwa chuo kitakachokiuka sheria na miongozo ya udhibiti wa ubora.

Alisema kutokana na changamoto za ubora zilizobainishwa na ukaguzi uliofanywa na Tume, na kwa kuzingatia umuhimu wa kuwa na wahitimu wenye kukidhi viwango bora vya elimu, wamefuta usajili wa kituo cha Moshi mjini cha Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo).

Alisema wanafunzi wa SMMUCo wanaoendelea na masomo watahamishiwa kampasi kuu ya chuo hicho iliyopo Masoka Moshi mkoani Kilimanjaro.

Alisema pia wamezuia udahili wa wanafunzi wapya na kuamuru kuhamishwa wale wa shahada ya kwanza wanaoendelea na masomo kwa mwaka 2018/19 katika programu tisa kwenye vyuo vikuu vinne.

Wanafunzi hao ni pamoja na wale wanaosomea shahada ya tiba na upasuaji na shahada ya sayansi ya uuguzi katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) cha Dar es Salaam.

Pia wameagiza kuhamishwa kwa wanafunzi wote wanaosomea udaktari wa binadamu kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu James (Ajuco) kilichopo Songea mkoani Ruvuma.

Wengine ni wanafunzi wanaosomea shahada ya sanaa na mawasiliano ya umma na ile ya sanaa na utawala kutoka SMMUCo Moshi.

Vilevile wamo wanafunzi wanaosomea shahada ya elimu na mahitaji maalumu (sanaa), shahada ya elimu na mahitaji maalumu (sayansi), shahada ya sayansi na elimu pamoja na shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (Sekomu) kilichopo Lushoto mkoani Tanga.

Alisema TCU pia imeridhia ombi la SMMUCo kuwahamisha wanafunzi katika programu za masomo ya utalii, diploma ya mawasiliano ya umma na cheti cha mawasiliano ya umma.

Profesa Kihampa alisema wameendelea kusitisha udahili wa wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Mtakatifu Fransisco (SFUCHAS) kilichopo Ifakara, Morogoro na Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo (AMUCTA) Tabora.

“Kumekuwa na sababu mbalimbali, lakini zinazojirudia ni uwiano wa wahadhiri na miundombinu kutokidhi hadhi ya kuwa chuo kikuu,” alisema.