Kamati ya Bajeti Zanzibar yazuru MCL

Muktasari:

Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar leo Alhamisi imetembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, MwanaSpoti na The Citizen

Dar es Salaam. Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar leo Alhamisi Novemba 15, 2018 imetembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) zilizopo Tabata relini jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wake, Mohamed Said Mohamed akizungumza ofisini hapo amesema kamati hiyo imefanikiwa kupatikana kwa matumizi bora ya fedha visiwani Zanzibar kwa kutoa ushauri wa namna ya kuziba mianya ya kupotea kwa mapato ya Serikali.

“Tumeanzisha vyanzo vipya vya mapato ikiwamo wanaoagiza magari wanapobadili nyaraka kuwa kwenye umiliki wao kulipa gharama kiasi.

“Mbali na hilo kuweka namba binafsi kulipia kutoka gharama iliyokuwa awali ya Sh5 milioni tano na kufikia Sh15 milioni,” amesema Mohamed.

Amesema kamati yake imeishauri Serikali itafute njia mbadala ya kuwafanya watalii waweze kulipia gharama za mazingira ambazo kila anayeingia hulipa dola moja.

Amesema jitihada za kuhakikisha kituo kimoja cha kutolea huduma kinakamilika.

“Kila kitu kipo sawa, bado mambo mawili matatu kutoka kwa Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (Zipa), kukubaliana lakini wawakilishi wa idara zote zinazohusika na biashara wana wawakilishi wao pale, ili mwekezaji anapokuja asipate tabu ya kuhangaika kukusanya nyaraka, badala yake kila kitu akipate katika eneo moja,” amesema Said Mohamed.

Kuhusu kuwa na eneo huru la uwekezaji Zanzibar, mwenyekiti huyo amesema bado ni changamoto kutokana na bidhaa zinazoingia Tanzania Bara zilizozalishwa Visiwani zinatozwa ushuru, ilihali za Bara zinaingia bila kutozwa.

Amesema suala hilo wamekuwa wakilijadili ana na kwa sasa wamewaachia mawaziri wa wawili wa bara na visiwani kulijadili na kuja na jibu lenye tija.

Kuhusu uhaba wa sukari mwenyekiti wa kamati hiyo amesema kuna mpango maalumu wamewekewa wafanyabiashara wa Zanzibar wanaopeleka sukari visiwani humo, lazima kwanza wanunue ya Mahonda na sukari ya nje hairuhusiwi kuuzwa.

Akizungumzia upungufu wa mafuta amesema tatizo linasababishwa na uhaba wa meli kwa sababu hadi sasa ipo moja nyingine iliyobaki imeharibika.

Naye Said Mohamed pia amezungumzia siasa za Visiwani kwa kusema licha ya chama kikuu cha upinzani CUF kuwa nje ya Baraza la Wawakilishi, vyama vitatu vilivyopo na chama tawala wanaisukuma serikali kwa kuhoji na kukosoa bila woga.

Amesema hata kukiwa na chama kimoja Baraza la Wawakilishi linaweza kufanya kazi ya kuisimamia Serikali ili itatue kero na changamoto za wananchi.