AfDB yaimwagia Tanzania mabilioni

Muktasari:

Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) imeipatia Tanzania mkopo kwa ajili ya kusaidia usambazaji umeme na kukabiliana na sumu kuvu kwenye nafaka

Dar es Salaam. Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeipatia Tanzania Sh486.5 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi miwili na kusaidia bajeti kuu.

 

Kati ya fedha hizo, Sh45 bilioni ni msaada na Sh440.7 bilioni ni mkopo wa masharti nafuu utakaolipwa ndani ya miaka 40.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James akizungumza leo Alhamisi Novemba 15, 2018 jijini Dar es Salaam amesema fedha hizo zitatumika kwenye mradi wa umeme na kukabiliana na sumu kuvu katika mahindi na karanga.

 

Kwa upande wa umeme, James amesema itajengwa njia ya kusafirishia umeme wa msongo mkubwa kutoka Nyakanazi hadi Kigoma wa Kv400.

Amesema mradi huo utauwezesha mkoa wa Kigoma kuingia kwenye gridi ya taifa na kupata umeme wa Taifa.

 

“Ukanda wa magharibi kila kitu kilikuwa nyuma lakini sasa umeme mkubwa huo unaenda na ipo mipango pia ya kutengeneza barabara,” amesema.

 

Kuhusu sumu kuvu, katibu mkuu huyo ameeleza kuwa  imebainika ni tatizo kubwa, hivyo Wizara ya Kilimo ilihitaji fedha kwa ajili mikakati mbalimbali iliyoweka kukabiliana na tatizo hilo.