Biashara ya majeneza Moshi yazua mjadala

Muktasari:

  • Huduma ya kununua jeneza kabla ya kifo imeibua mjadala mjini Moshi, Mchungaji Samwel Msack amewashangaa wanaoogopa kununua majeneza wakiwa hai kwani majeneza hayo hayo yatawasubiri tu barabarani ingawa wengine wamefananisha kitendo cha kununua jeneza ukiwa hai na wendawazimu

Moshi. Wakati baadhi ya wafanyabiashara wakibuni mbinu za kuvutia wateja, wauza majeneza katika eneo la Hospitali ya KCMC mjini hapa wamedai biashara hiyo kwa sasa ni ngumu na imevamiwa jambo lililosababisha ushindani mkubwa.

Wafanyabiashara hao wameenda mbali na kudai punguzo la aina tofauti lililowekwa na kampuni ya Godmark Funeral Directors, maarufu kama vifurushi, haliwezi kuwaathiri kibiashara kwa kuwa wanatofautiana kwa huduma na bei. Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika eneo hilo, wafanyabiashara hao walisema biashara hiyo imevamiwa na watu wengi na sasa wamefikia zaidi ya watu 20 wanaofanya biashara hiyo katika mji wa Moshi.

Monica Francis, mmoja wa wauzaji wa majeneza katika eneo hilo alisema kwa sasa wanafanya biashara hiyo kwa kujulikana.

“Ambao hawajulikani wanaweza kukaa hadi miezi miwili bila ya kuuza jeneza hata moja,” alisema.

“Unavyojulikana na unavyohudumia vizuri wateja ndivyo unavyoweza kupata wateja,” alisema Francis.

Naye mfanyabiashara mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema kutokana na biashara kuwa ngumu, wanaweza kukaa hata miezi miwili hawajauza jeneza hata moja.Walisema punguzo la asilima 30 kwa jeneza lililotolewa na kampuni ya Godmark kwa mteja ambaye ananunua kabla ya kufariki, haliwezi kuwaathiri kwa kuwa bei hutokana na ubora wa majeneza.

Monica Francis alifafanua kuwa gharama na ubora wa majeneza katika kampuni ya Godmark ni za juu hivyo ni vigumu kushindana nao kwa kuwa wako kwenye soko muda mrefu.

“Hivyo wateja wetu bado wataendelea kuwepo hata punguzo hilo likiwepo,” alisema Francis.

Wakati Francis akieleza hayo, mfanyabiashara mwingine alisema Godmark inatoa huduma zote za mazishi ikiwa ni pamoja na kusafirisha maiti, hivyo wao hawawezi kushindana nayo.

Alisema kwa utamaduni ulivyo hasa kwa watu wa Kilimanjaro, ni ngumu kununua majeneza wakiwa bado hai. “Hilo bado ni gumu hasa kwa Kilimanjaro, labda kwa wasomi sana,” alisema.

Katika eneo hilo, wafanyabiashara hao huuza majeneza kati ya Sh100,000 na Sh450,000 wakati Godmark huuza kuanzia Sh390,000 hadi Sh1.5 milioni.

Punguzo laibua mjadala

Wakati wafanyabiashara wakionyesha kutoyumbishwa na punguzo hilo, wananchi mjini Moshi walitofautiana kuhusu huduma hiyo ya kununua jeneza kabla ya kufariki, baadhi wakisema ni jambo zuri.

Mchungaji Samwel Msack wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), alisema wanaokataa kununua jeneza wakiwa hai haiwasaidii chochote kwa kuwa bado yatawasubiri barabarani.

“Mtu anakataa kununua jeneza akiwa hai, lakini si bado yako hapo barabarani kuelekea KCMC yanamsubiri? Hii haina tofauti na Yerusalemu (ambako) unakuta makaburi yako tayari?” alihoji.

“Hata kwenye Biblia, Abraham, baba wa imani, alinunua shamba la kuzikiwa yeye, familia yake na ndugu zake kwa shekeli 400 kutoka kwa Banheth. Mbona hakufa hapohapo?” alihoji.

Mkazi wa Tarakea wilayani Rombo, Yusuph Mruma, ambaye ni ofisa mstaafu wa Jeshi la Polisi, alisema japokuwa kila mtu anajua atakufa, kununua jeneza ukiwa hai ni wendawazimu.

“Mimi sitakaa nifanye hicho kitu. Kila mtu anajua atakufa, lakini kuandaa leo jeneza lako hapana hilo nakataa. Yaani leo ninunue jeneza niingize ndani lisubiri nife? Hapana,” alisema.

Kwa siku nzima ya jana kulikuwa na mijadala katika mitandao ya kijamii baada ya gazeti hili kuchapisha taarifa maalumu juu ya punguzo la asilimia 30 kwa mtu anayenunua jeneza akiwa hai.

Katika kundi moja la Whatsapp, mchangiaji mmoja aliandika: ”Zamani ilikuwa ni uchuro kutengeneza jeneza kabla, baadaye ikawa ni biashara ya kawaida. Lakini sasa hivi kuna hadi kibao cha karibu tena.”

Mchangiaji mwingine aliandika akisema “nikifa watakaobaki watajua pa kuniweka”, huku mwingine akiandika”biashara nyingine ni ibilisi. Utanunuaje jeneza ukiwa hai?”

Mbali na wachangiaji hao lakini mwingine akaandika” Hiyo nzuri sana. Hizi ni nyakati za mwisho tena enzi hizi mwendo wa viroba na banana ni bora ukanunua jeneza lako mapema”.