Waziri ataka uhakiki wa mizani inayopima korosho

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda

Muktasari:

  • Serikali imesema kuna changamoto katika mizani inayotumika kupima korosho hali inayosababisha baadhi ya wakulima kuibiwa

Mtwara. Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda ameagiza wakala wa vipimo na mizani nchini kutembelea maeneo yote yanayohusika na ukusanyaji na upimaji korosho kuangalia vipimo vyote na kujiridhisha kama vinakubalika kisheria.

Kakunda ametoa agizo hilo leo Jumapili Desemba 9, 2018 katika kikao maalumu cha kuzungumza na wabanguaji wadogo wa korosho kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuingia nao makubaliano ya kubangua korosho zinazonunuliwa na Serikali.

Amesema wapo watakaohoji kwa nini yeye ametoa maagizo hayo na kufafanua kwamba, wizara yake na Wizara ya Kilimo zinashirikiana katika mambo mengi na zimepewa dhamana sawasawa na watoto pacha.

“Wakala wa vipimo na mizani watembelee maeneo yote waangalie vipimo na wajiridhishe, kipimo cha nusu kilo kama kinakubalika kisheria hakiwezi kukataliwa na mtu yeyote kwa hiyo wakapime waandae taarifa yao,” amesema Kakunda.

Wakati wa kupokea maoni na ushauri kutoka kwa wabanguaji hao mmoja wa wabaguaji, Siwa Rajabu amedai kuwa katika vyama vya msingi  kuna tatizo la mizani kwani kipimo cha nusu kilo hakipo.

“Ni mizani gani katika nchi hii ya usawa haisomi nusu kilo. Ukipeleka korosho ghalani huruhusiwi kusogelea mzani, tunaomba Serikali inunue mizani ya elektroniki ili hata gramu kadhaa zikizidi mkulima apatiwe haki yake kwani hivi sasa hata kama utapima nyumbani ukifikisha ghalani unakuta kuna kilo zinapungua,” amesema Rajabu.

Awali, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema mizani katika vyama vya ushirika ni changamoto kubwa na wakulima wengi wanaibiwa sana.

“Unakuta korosho zinatoka chama fulani cha ushirika na majina yameambatanishwa na kiwango chake, ukienda chama kikuu cha ushirika ambao nao wana taarifa hizohizo utakuta kilo zinazosomeka katika chama kikuu ni tofauti na zinazosomeka katika chama cha msingi,” amesema Hausnga.